Sudan yamtimua ofisa wa UN kwa kuandaa ripoti 'bandia' juu ya Darfur
(last modified Thu, 26 May 2016 07:41:56 GMT )
May 26, 2016 07:41 UTC
  • Sudan yamtimua ofisa wa UN kwa kuandaa ripoti 'bandia' juu ya Darfur

Sudan imemtimua ofisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa nchini humo kwa tuhuma za kuandaa kile kilichotajwa na serikali ya Khartoum kuwa ripoti bandia kuhusu hali ya kiusalama katika eneo la Darfur.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya UN, serikali ya Khartoum imekataa kurefusha kibali cha kumruhusu Ivo Freijsen, Mkuu wa Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA kuhudumu nchini humo baada ya muda wa leseni yake kutamatika hapo Juni 6.

Akitetea uamuzi huo, Ibrahim Ghandour , Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan amesema ofisa huyo wa Umoja wa Mataifa 'alitia chumvi' ripoti aliyoiandaa kuhusu machafuko na hali ya kiusalama katika eneo la Darfur. Ameongeza kuwa, Mkuu huyo wa Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa alisema katika ripoti yake kuwa watu zaidi ya laki moja wamefurushwa makwao kutokana na machafuko katika eneo hilo, ilihali takwimu rasmi za serikali zinaonyesha kuwa ni watu 11,000 pekee ndio waliolazimika kuhama, mbali na kutangaza kuwa Sudan inakabiliwa na baa la njaa, jambo ambalo limekanushwa vikali na serikali ya Khartoum. Sudan inamtuhumu ofisa huyo kuwa amekuwa akikataa kutoa ushirikiano kwa maafisa wa serikali ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, tangu mwaka 2003 eneo la Darfur limekuwa likishuhudia mapigano ya waasi wanaopinga ubaguzi wa Rais Omar al-Bashir wa Sudan, mapigano ambayo yanaendelea hadi leo.