Rais wa Gambia awataka wapinzani waheshimu uamuzi wa mahakama
(last modified Wed, 29 Dec 2021 07:44:33 GMT )
Dec 29, 2021 07:44 UTC
  • Rais wa Gambia awataka wapinzani waheshimu uamuzi wa mahakama

Rais Adama Barrow wa Gambia ametoa mwito kwa upinzani nchini humo kukubali na kuheshimu uamuzi wa jana Jumanne wa Mahakama ya Juu ya nchi hiyo wa kutupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyompa ushindi kiongozi huyo.

Barrow alisema hayo jana muda mfupi baada ya Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kutupilia mbali faili la kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais lililowasilishwa na mpinzani wa karibu wa Barrow katika uchaguzi huo wa hivi karibuni, Ousainou Darboe.

Rais wa Gambia ameeleza bayana kuwa, "nauomba upinzani ukubali uamuzi wa Mahakama ya Juu pasi na masharti yoyote. Washindani wangu wametumia njia zote (kupinga ushindi wangu), na sasa wanapaswa kujiunga na kambi (iliyoshinda) kujenga taifa."

Hapo jana, Mahakama ya Kilele ya Gambia ilifutilia mbali ombi la kinara wa chama cha United Democratic Party (UDP) la kutaka uchaguzi wa rais ubatilishwe, kutokana na sababu za kiufundi.

Rais Barrow (kushoto) na mpinzani wake mkuu wa kisiasa

Uamuzi huo wa Mahakama ya Juu ya Gambia ni wa mwisho na wala hauwezi kukatiwa rufaa. 

Barrow ambaye ushindi wake katika uchaguzi wa rais miaka mitano iliyopita ulimaliza miongo miwili ya utawala wa kidikteta wa Yahya Jammeh alishinda kipindi cha pili cha uchaguzi wa rais kwa kupata zaidi ya silimia 53 ya kura. Mpinzani wake wa karibu Ousainou Darboe alipata asilimia 27.7 ya kura kwa mujibu wa tangazo la tume ya uchaguzi, mapema mwezi huu wa Disemba.