Wanajeshi wa Burundi 'waonekana' mashariki mwa Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78874-wanajeshi_wa_burundi_'waonekana'_mashariki_mwa_kongo_dr
Wanajeshi wa Burundi wameripotiwa kuingia katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 05, 2022 23:20 UTC
  • Wanajeshi wa Burundi 'waonekana' mashariki mwa Kongo DR

Wanajeshi wa Burundi wameripotiwa kuingia katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Chifu wa eneo la Lemera, Edmond Simba Muhogo aliliambia shirika la habari la AFP jana Jumatano kuwa, vikosi vya Burundi viliingia katika eneo hilo la mashariki mwa DRC Jumapili iliyopita.

Amesema makomandoo hao wa Burundi wapatao 380 wameingia nchini Kongo DR kupitia wilaya ya Lemera iliyoko katika eneo la Uvira mkoani Kivu Kusini, kwa shababa ya kukabiliana na waasi wa Kirundi.

Chifu huyo amesema wanajeshi wa Burundi kwa sasa wanakabiliana na kundi sugu la waasi wanaobeba silaha katika wilaya za Bijojo na Bibangwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kundi hilo la waasi linalojiita RED-Tabara, lenye wapiganaji kati ya 500 na 800, na lenye makao yake mashariki mwa DRC, limekuwa likifanya mashambulizi ya kuvizia ndani ya Burundi tokea mwaka 2015.

Magenge ya waasi DRC

Willy Siremba, mwakilishi wa makundi ya kiraia katika eneo la Uvira, ameitaka serikali ya DRC ijitokeze wazi na iwaeleze wananchi kuhusu uwepo wa vikosi hivyo vya kigeni ndani ya ardhi ya nchi yao.

Julai mwaka jana, Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alifanya mazungumzo mjini Kinshasa na Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi, ambapo suala la usalama wa mashariki mwa DRC lilitawala mazungumzo hayo, kufuatia kuwepo kwa makundi yenye silaha kutoka Burundi yaliyokimbilia mkoa wa Kivu Kusini.