Iran kutoenda Hijja mwaka huu kutokana na vizingiti vya Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8065-iran_kutoenda_hijja_mwaka_huu_kutokana_na_vizingiti_vya_saudia
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema taifa hili halitashiriki ibada tukufu ya Hijja mwaka huu kutokana na vizingiti lilivyowekewa na Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 29, 2016 14:21 UTC
  • Iran kutoenda Hijja mwaka huu kutokana na vizingiti vya Saudia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema taifa hili halitashiriki ibada tukufu ya Hijja mwaka huu kutokana na vizingiti lilivyowekewa na Saudi Arabia.

Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran amewaambia waandishi wa habari mjini Tehran kuwa "Ni wazi kwamba taifa hili halitaenda kutekeleza ibada ya Hijja mwaka huu baada Saudia kuliwekea vizingiti na kushindwa kushughulikia matakwa yake."

Amesema duru mbili za mazungumzo kati ya Riyadh na wajumbe wa Tehran ya kujaribu kuyatafutia ufumbuzi matakwa ya Iran na haswa wasi wasi wa nchi hii juu ya usalama wa Mahujaji hazikuzaa matunda na kwamba leo ilikuwa siku ya mwisho kwa utawala wa Aal-Saudi kutatua hitilafu hizo. Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ilihisi kuwa ina jukumu na wajibu wa kuelezea hofu yake juu ya usalama wa Mahujaji haswa ikizingatiwa kuwa, Mahujaji zaidi ya 4,000, ambapo 460 miongoni mwao walikuwa raia wa Iran, waliaga dunia kutokana na usimamizi mbaya wa ibada hiyo tukufu katika eneo la Mina mwaka jana. Kauli ya Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran yanajiri siku moja baada ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kusema kuwa, Saudi Arabia imeifungia Iran njia zote na kwamba inapasa kulaumiwa iwapo Waislamu watashindwa kwenda Hija mwaka huu. Jaberi Ansari aliashiria jana usiku kuhusu Hija ya mwaka huu na kuongeza kuwa, Saudia inalihusisha suala la Hija na masuala ya kisiasa tofauti na maneno inayotoa hadharani.