UN: Raia 440 wameuawa katika mapigano nchini Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i80942-un_raia_440_wameuawa_katika_mapigano_nchini_sudan_kusini
Umoja wa Mataifa umesema, raia wasiopungua 440 wameuawa katika mapigano makali kati ya pande hasimu kusini-magharibi ya Sudan Kusini ndani ya kipindi cha miezi michache katika mwaka uliopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 02, 2022 10:20 UTC
  • UN: Raia 440 wameuawa katika mapigano nchini Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umesema, raia wasiopungua 440 wameuawa katika mapigano makali kati ya pande hasimu kusini-magharibi ya Sudan Kusini ndani ya kipindi cha miezi michache katika mwaka uliopita.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na mauaji hayo imetolewa kufuatia indhari ya mwezi uliopita ya taasisi hiyo kuu kimataifa kwamba taifa hilo changa zaidi duniani liko hatarini kurejea tena kwenye janga la vita, kutokana na machafuko ya kikabila na makabiliano ya kisiasa kutishia kurejesha nyuma hatua chache zilizopigwa katika utekelezaji wa mchakato wa amani katika nchi hiyo.

Ripoti hiyo ya pamoja iliyotolewa Jumanne na Mpango wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini (UNMISS) na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imeeleza kuwa, unyanyasaji na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, yakiwemo mauaji ya mamia ya watu yamefanywa dhidi ya raia wakati wa mapigano yaliyotokea kwenye eneo la Tambura katika jimbo la Equatoria Magharibi.

Rais Salva Kiir (kushoto) na makamu wake Riek Machar

Ripoti hiyo imewalaumu na kuwahusisha na mauaji hayo wanamgambo wa vikosi vitiifu kwa Rais Salva Kiir na wa mahasimu wake katika upinzani wa Harakati na Jeshi la Ukombozi la Watu wa Sudan (SPLM/A-IO) wanaoongozwa na Makamu wa Rais Riek Machar.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imebaini kuwa, raia wasiopungua 440 waliuawa, 18 walijeruhiwa na wengine 74 walitekwa nyara kati ya Juni na Septemba 2021, katika mapigano baina ya pande hasimu kwenye eneo la Tambura.

Kadhalika, raia wasiopungua 64 walifanyiwa unyanyasaji wa kingono uliohusishwa na mapigano hayo akiwemo msichana wa miaka 13 aliyebakwa genge la watu hadi kufa, mbali na watu wasiopungua 56 walioripotiwa kutoweka katika kipindi cha Juni hadi Septemba. 

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, watu wapatao 80,000 walilazimika kuyahama makazi yao ili kuepuka mapigano.../