Bunge la Misri lakosolewa kwa kuunga mkono serikali ya al Sisi
Mwanasiasa mwandamizi wa Misri amelikosoa Bunge la nchi hiyo akisema Wamisri hawana matumaini na bunge hilo kutokana na misimamo yake ya kuiunga mkono serikali ya Jenerali Abdul Fattah al Sisi.
Ahmad Fauzi ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu la chama cha Demokrasia nchini Misri amesema Bunge la sasa la nchi hiyo ni bunge la serikali na haliwezi kupinga au kukosoa maamuzi yoyote kwa sababu limekuja madarakani kwa ridhaa ya serikali ya sasa ya Cairo.
Ahmad Fauzi amongeza kuwa Rais Abdul Fattah al Sisi wa Misri amekuwa akitumia mbinu za ukandamizaji na za kidikteta dhidi ya uhuru wa wananchi kwa kuhofia mapinduzi mengine ya wananchi na kwamba Bunge nalo limetupilia mbali kazi yake ya kutetea uhuru wa wananchi kwa sababu ya kuiunga mkono serikali ya Cairo. Amesema kuwa mbinu za kipolisi zinazotumiwa na serikali kukabiliana na wananchi zimezidisha machafuko na ukosefu wa amani.
Mamia ya wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani wa Misri, Muhammad Morsi, wamekamatwa na kuhukumiwa kifo nchini Misri, suala ambalo Umoja wa Mataifa umesema halina mfano katika historia ya sasa ya dunia. Vilevile jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu zimetangaza kuwa ukandamizaji unaofanywa na serikali ya Abdul Fattah al Sisi ni mkubwa zaidi kuliko ule wa kipindi cha dikteta Hosni Mubarak.