Tanzania: Wakaazi wa kijiji kulikojiri mauaji Tanga wahama
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8398-tanzania_wakaazi_wa_kijiji_kulikojiri_mauaji_tanga_wahama
Wakaazi wa kijiji cha Kibatini mkoani Tanga huko Tanzania wamekihama kijiji chao kufuatia mauaji ya kutisha yaliyotokea katika eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 03, 2016 10:14 UTC
  • Tanzania: Wakaazi wa kijiji kulikojiri mauaji Tanga wahama

Wakaazi wa kijiji cha Kibatini mkoani Tanga huko Tanzania wamekihama kijiji chao kufuatia mauaji ya kutisha yaliyotokea katika eneo hilo.

Duru zinaarifu kuwa, wasiwasi umetanda katika kijiji hicho baada ya watu wanane kutoka kijiji cha Kibatini kwenye kata ya Amboni kuchinjwa kama wanyama na watu wasiojulikana Jumatatu usiku. Taarifa zinasema kuwa, wanakijiji 70 wameshaondoka katika kijiji cha Kibatini, Wadi ya Mzizima na kuhamia kijiji cha Corner Z katika wadi hiyo. Wanakijiji hao wamehama makazi yao kwa kuhofia maisha yao hata baada ya polisi kuwahakikishia usalama wao. Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbaruk (CUF), amelazimika kukatisha vikao vya Bunge vinavyoendelea Dodoma na kwenda kuwahamisha wananchi wa Kibatini baada ya kutokea mauji ya watu wanane. Mbunge huyo amesema anaungana na wapiga kura wake akisema kwa sasa eneo hilo si salama kwa maisha. Sheikh wa Mkoa wa Tanga, Ali Juma Luuchu, aliiomba Serikali kushirikisha viongozi wa dini na wazee kutafuta suluhu ya kudumu ya matukio hayo yanaonekana kutamalaki katika jiji hilo. Alisema tukio hilo haliwezi kuachiwa serikali pekee kwa vile ni lazima wao kama viongozi wa dini washirikiane na kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa kwa sababu vinachafua sura ya mkoa wa Tanga na nchi kwa ujumla. Katika wiki za hivi karibuni watu kadhaa wameuawa kinyama kwenye maeneo mbalimbali Tanzania huku wananchi wakiingiwa na hofu na kuitaka serikali ichunguze sababu ya kuzorota usalama. Serikali ya Tanzania imesema kutuma kikosi maalumu cha ulinzi, kikiongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kuwasaka watu wanaoaminika kufanya mauaji hayo mkoani Tanga.