S/Kusini yabuni kamati ya kuanisha hatima ya majimbo 28
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8437-s_kusini_yabuni_kamati_ya_kuanisha_hatima_ya_majimbo_28
Sudan Kusini imebuni kamati maalumu ya kuanisha hatima ya majimbo 18 ya ziada yaliyotangazwa mwishoni mwa mwaka uliopita 2015 na Rais Salva Kiir.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 04, 2016 03:13 UTC
  • S/Kusini yabuni kamati ya kuanisha hatima ya majimbo 28

Sudan Kusini imebuni kamati maalumu ya kuanisha hatima ya majimbo 18 ya ziada yaliyotangazwa mwishoni mwa mwaka uliopita 2015 na Rais Salva Kiir.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Juba jana Ijumaa, Makamu wa Kwanza wa Rais Dakta Riek Machar na wa Pili James Wani Igga walisema kamati hiyo inajumuisha wawakilishi wa vyama vyote vikuu vya siasa nchini. Dakta Machar amesema kamati hiyo inawaleta pamoja wajumbe 10 wa vyama vikuu vya siasa pamoja na wawakilishi wengine 5 kutoka jamii ya kimataifa, huku akibainisha kuwa wataziomba Tanzania na Afrika Kusini zitume wajumbe wawili. Amesema kamati hiyo ya watu 15 itapewa siku 30 kuangalia upya idadi ya majimbo mapya, kuanisha mipaka yake na kuja na mapendekezo ya iwapo majimbo hayo mapya yatasalia au yataondolewa.

Disemba mwaka jana, RAIS Salva Kiir alivunja majimbo 10 ya nchi hiyo na badala yake kuunda majimbo 28 mapya na kutoa orodha ya magava wa majimbo hayo, hatua ambayo ilihatarisha makubaliano ya amani ya Agosti mwaka jana.

Mbali na swala hilo la majimbo, Dakta Riek Machar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini amesema Rais Salva Kiir amekubali kadhia ya kuachiwa huru wafungwa wa kivita na kisiasa.

Haya yanajiri siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kusema Sudan Kusini ipo katika ncha ya kuwekewa vikwazo vipya na jamii ya kimataifa kutokana na mwendo wa kinyonga wa kutekeleza makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka jana.