NEC Tanzania: Hatukuwataka waangalizi wa uchaguzi kuangalia wa ZNZ ila wa bara
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8491-nec_tanzania_hatukuwataka_waangalizi_wa_uchaguzi_kuangalia_wa_znz_ila_wa_bara
Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) imetoa radiamali yake juu ya ripoti ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana 2015, iliyowasilishwa hivi karibuni na ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 05, 2016 00:07 UTC
  • NEC Tanzania: Hatukuwataka waangalizi wa uchaguzi kuangalia wa ZNZ ila wa bara

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) imetoa radiamali yake juu ya ripoti ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana 2015, iliyowasilishwa hivi karibuni na ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU).

Katika radiamali yake NEC imesema kuwa ripoti hiyo imebainisha mapungufu ambayo hayamo kwenye sheria na taratibu zinazofuatwa na tume hiyo. Akiongea na waandishi wa habari kuhusu ripoti hiyo, mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania, Ramadhan Kailima amesema kuwa, kwa mujibu wa sheria, waliwapa nafasi hiyo waangalizi wa ndani na nje ili kuangalia na kufuatilia uchaguzi wa Tanzania bara, kama unaenda kulingana na katiba, sheria na taratibu za uchaguzi huo. Ameongeza kuwa katika ripoti hiyo, waangalizi hao wamezungumzia uchaguzi wa Zanzibar, ambao NEC hawahusiki nao na kwamba wamefanya makosa, hasa kwa kuzingatia kuwa wao walikuwa waangalizi wa uchaguzi wa Tanzania bara tu na sio visiwani Zanzibar. Miongoni mwa mapungufu waliyoyaeleza waangalizi hao wakiwakilishwa na Mwangalizi Mkuu wa Ujumbe wa Waangalizi wa EU, Bi. Judith Sargentini na kuitaka serikali ya Tanzania kuyafanyia kazi ni pamoja na suala zima la uchaguzi wa Zanzibar, kuangaliwa upya sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 na kuwepo kwa haki ya wagombea binafsi kugombea nafasi yoyote katika uchaguzi wowote wa Tanzania bara na Zanzibar, mgawanyo wa majimbo na uwazi wa kuhesabu kura. ‘’Waangalizi wowote wa uchaguzi wanapoomba kibali kuangalia uchaguzi, wanatakiwa kufuata taratibu kwa kutambua kwamba kuna NEC na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Hawakupaswa kuingiza kwenye ripoti yao masuala ya uchaguzi wa Zanzibar na badala yake wangeeleza kama NEC hatukufuata sheria na taratibu kwenye uchaguzi huu wa Tanzania bara.’’ Alisema Kailima.