Rais wa Somalia apatwa na COVID-19 baada ya kuitembelea Imarati
Rais wa Somalia amesema amejiweka karantini baada ya kugundua kuwa ameambukizwa ugonjwa wa COVID-19.
Rais Hassan Sheikh Mohamud amebainika kupatwa na maradhi ya Corona muda mfupi baada ya kuutembelea Muungano wa Falme za Kiarabu, katika safari yake ya kwanza nje ya nchi.
Katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter jana Ijumaa, Rais wa Somalia amesema: Kufikia sasa sina dalili zozote, lakini nitaendelea kujitenga na kulihudumia taifa la Somalia nikiwa nyumbani.
Amewataka wananchi wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika wawe makini, na wazingatie miongozo na protokali za afya zilizoainishwa na watalaamu wa afya nchini humo.
Hassan Sheikh Mohamud mwenye umri wa miaka 66 na ambaye aliwahi kuiongoza Somalia huko nyuma, kati ya mwaka 2012 na 2017, alirejea nchini jana Ijumaa akitokea Imarati, katika ziara yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa Mei 15.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani, nchi hiyo ya Kiafrika imerekodi kesi 26, 748 za ugonjwa wa COVID-19 mpaka sasa, huku watu 1, 361 wakiaga dunia kutokana na maradhi hayo.