Jul 18, 2022 02:30 UTC
  • Algeria yapinga tena mpango wa utawala wa ndani Sahara, yaishutumu Rabat kwa udanganyifu

Algeria mepinga tena mpango wa kuanzisha utawala wa ndani uliopendekezwa na Morocco kwa ajili eti ya kutatua mzozo wa eneo la Sahara Magharibi linalozozaniwa kati ya Morocco na Harakati ya Polisario.

Barua iliyotumwa na mwakilishi wa Algeria katika Umoja wa Mataifa, Nazir Arbaoui kwa Baraza la Usalama la umoja huo, ambayo imechapishwa kujibu taarifa za awali za balozi wa Morocco katika Umoja wa Mataifa, imetoa maelezo ya msimamo wa Algeria na ukweli kuhusiana na mkondo wa kihistoria ya suala la Sahara, ikilitaja pendekezo la Morocco kuwa ni "jaribio la kulazimisha hali iliyopo sasa katika eneo la Sahara Magharibi.

Balozi Arbaoui ameonya kwamba maudhui, misingi na malengo ya kile kinachoitwa 'utawala wa ndani' katika eneo la Sahara Magharibi ni hatari ambayo inatishia msingi wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Amesema kwamba "kukubali hali inayotawala sasa huko Sahara Magharibi yaani uvamizi wa Morocco kwa jina la utawala wa ndani wa eneo hilo, kutakuwa na maana ya jumuiya ya kimataifa kuhalalisha uvamizi na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya taifa jingine; suala ambalo itakuwa mara ya kwanza kufanywa na Umoja wa Mataifa tangu kuasisiwa kwa taasisi hiyo ya kimataifa.

Balozi wa Algeria katika Umoja wa Mataifa amsema, Rabat inazuia kwa makusudi ujumbe wa umoja huo kutekeleza majukumu yake ya kusimamia hali ya haki za binadamu katika maeneo ya Sahara Magharibi inayokaliwa kwa mabavu. Amesema Morocco inazuia utatuzi wa amani wa mzozo huo unaolenga kupata suluhisho la haki na la kudumu ambalo linawahakikishia watu Sahara Magharibi kupata haki yao ya kujitawala.

Mgogoro wa Sahara Magharibi ulianza mwaka 1975 baada ya kufurushwa wakoloni wa Uhispania katika eneo hilo.

Watu wa Sahara Magharibi wanapinga uvamizi wa Morocco

Morocco ililiteka eneo hilo, lakini harakati ya Polisario ambayo iliundwa mwaka 1973 ili kupambana na wakoloni wa Uhispania, inasema kuwa Sahara Magharibi ni nchi huru inayokaliwa kwa mabavu na Morocco.

Kwa sasa, Morocco inadhibiti asilimia 80 ya eneo la Sahara Magharibi huku sehemu iliyosalia ikishikiliwa na Harakati ya Polisario inayoungwa mkono na Algeria. Kwa miaka 15, Polisario imepigana vita na Morocco vya kulikomboa eneo hilo, baada ya Uhispania kuondoa askari wake mwaka 1975 na inataka iitishwe kura ya maoni ya kuamua uhuru na kujitawala watu wa Sahara Magharibi.

Tags