Jul 18, 2022 07:38 UTC
  • Jeshi la Nigeria laua magaidi 46 wa ISWAP jimboni Borno

Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuwaangamiza wanachama 46 wa kundi la kigadi la ISIS Wilaya ya Afrika Magharibi (ISWAP) kaskazini mwa nchi.

Taarifa ya Jeshi la Nigeria imesema, mbali na kuuawa wanachama 46 wa kundi hilo la kigaidi katika operesheni ya anga iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika mji wa Damasak jimboni Borno kaskazini mashariki mwa nchi, makamanda sita wa genge hilo wamelazimika kujisalisha kwa vyombo vya ulinzi vya nchi hiyo.

Akiongea na waandishi wa habari mjini Abuja jana Jumapili, Meja Jenerali Benard Onyeuko, Murugenzi wa Vyombo vya Habari wa jeshi hilo amesema maficho ya magaidi hao katika miji ya Tumbun Jaki na Tumbun Murhu karibu na eneo la Ziwa Chad yameharibiwa kwa mabomu yaliyodondoshwa kutoka angani.

Ameleza kuwa, baadhi ya magaidi hao wameuawa licha ya kutorokea katika vichaka na misitu ya karibu, baada ya ngome zao kusambaratishwa kwa mabomu na maroketi.

Wanachama wa ISWAP waliokuwa sehemu ya Boko Haram

Katika miezi ya karibuni, maelfu ya wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram na wenzao wa ISWAP wamekuwa wakijisalimisha kwa maafisa usalama huko kaskazini mwa Nigeria.

Magaidi wakufurishaji wamekuwa wakitekekeza jinai kaskazini mwa Nigeria na nchi jirani za Chad, Niger na Cameroon na kupelekea makumi ya maelefu ya watu wasio na hatia kuuawa katika kipindi cha miaka zaidi ya 10 iliyopita huku mamilioni ya wengine wakiachwa bila makao.

Tags