Afrika Kusini: Tahadhari ya Marekani haina msingi wowote
Waziri wa Usalama nchini Afrika Kusini, David Mahlobo amesema kuwa, tahadhari ya kuwepo uwezekano wa kujiri hujuma ya kigaidi nchini humo ambayo imetolewa na serikali ya Marekani, haina msingi wowote.
Mahlobo ameyasema hayo katika radiamali yake kuhusiana na tahadhari iliyotolewa na viongozi wa Marekani juu ya uwezekano wa kujiri mashambulizi ya kigaidi mwezi wa Ramadhani nchini Afrika Kusini na kuongeza kuwa, hakuna hatari yoyote inayoikabili nchi hiyo kwa sasa na kwamba, tahadhari hiyo haina msingi wowote. Kabla ya hapo ubalozi wa Marekani nchini Afrika Kusini alikuwa ametangaza kuwa miji miwili ya Johannesburg na Cape Town ambayo imejaa idadi kubwa ya watalii wa kigeni wengi wao wakiwa ni raia wa Marekani, inakabiliwa na hatari ya kushambuliwa na magaidi, suala ambalo limekanushwa vikali na David Mahlobo.