Jun 07, 2016 07:33 UTC
  • Askari wa AMISOM wakamatwa kwa kuuza bidhaa za kikosi hicho

Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kinawazuilia askari wake watano wanaotuhumiwa kuuza kinyume cha sheria suhula na bidhaa za kikosi hicho.

Taarifa ya AMISOM imesema kuwa, askari hao walipatikana na fueli na mifuko ya kikosi hicho kinyume cha sheria, baada ya kukamatwa katika operesheni ya pamoja iliyohusisha kikosi hicho na polisi ya Somalia. Taarifa ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia imeongeza kuwa, watano hao watafunguliwa mashitaka ya kumiliki mali za AMISOM kinyume cha sheria na kwamba wamekiuka kanuni za kimaadili za kikosi hicho. Hata hivyo taarifa hiyo haijabainisha uraia wa washukiwa hao watano wa Kiafrika. Itakumbukwa kuwa, mwezi Aprili mwaka huu, Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kilitoa taarifa rasmi ya kuomba msamaha kwa kuua 'kimakosa' raia wanne wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Askari elfu 22 wa Afrika walitumwa nchini Somalia miaka 9 iliyopita kwa ajili ya kurejesha amani na kukabiliana na harakati za kundi la kigaidi la al-Shabaab.

Mbali na tuhuma za wizi, askari wa kulinda amani katika nchi nyingi na haswa za Kiafrika kama vile Jamhuri ya Afrika ya Kati, wamekuwa wakikabiliwa na madai ya ubakaji.

Tags