Jeshi la Somalia laua magaidi karibu 50 wa al-Shabaab katika mashambulizi 2
Jeshi la Somalia limewauwa magaidi 47 wa al-Shabaab katika mashambulizi mawili tofauti leo Alkhamisi, likiwemo lile la Aadan Yabaal katika eneo la Shabelle ya Kati, mji wa kimkakati uliotwaliwa na kundi hilo la kigaidi lenye mfungamano na al-Qaeda jana.
Wizara ya Habari ya Somalia imesema katika taarifa yake kwamba, shambulizi la anga dhidi ya Aadan Yabaal lilitekelezwa kwa msaada wa vikosi vya kigeni na lililenga mkusanyiko wa magaidi na maficho yao katika mji huo.
"Ripoti za awali zinaonyesha kuwa, wanachama 12 wa Khawaarij, wakiwemo viongozi wakuu, waliuawa. Muhimu zaidi, hakukuwa na majeruhi kwa upande wa raia," imesema taarifa hiyo.
Serikali ya Somalia hutumia neno "Khawaarij" kuashiria magaidi hususan wanachama wa genge la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab.
Kwa mujibu wa taarifa tofauti ya wizara, takriban magaidi 35 wa al-Shabaab waliuawa baada ya wanajeshi wa jimbo la Darwish, Kusini Magharibi kuzuia shambulio la al-Shabaab kwenye kambi ya jeshi nje kidogo ya mji wa Baidoa leo Alkhamisi.
Mashambulizi hayo ya anga yanakuja siku moja baada ya kundi la al-Shabaab kuuteka mji wa Adan Yabaal, yapata kilomita 245 kutoka mji mkuu, Mogadishu.
Mji huo wa kimkakati una umuhimu wa kijeshi na unatumika kama kitovu muhimu cha lojistiki, na unaunganisha jimbo la Hirshabelle na jimbo jirani la kati la Galmudug.
Wakati wa operesheni ya kijeshi mwaka 2022, jeshi la Somalia, likisaidiwa na wapiganaji wa ndani, liliukomboa mji huo kutoka mikononi mwa al-Shabaab.
Baadaye, mamia ya raia waliandamana katika mitaa ya jiji kuunga mkono vikosi vya serikali. Baidoa, mji mkubwa zaidi katika Jimbo la Kusini Magharibi, uko umbali wa kilomita 245 (maili 152) kusini magharibi mwa Mogadishu.