Baada ya Marekani, UK nayo yatahadharisha shambulio la kigaidi Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8713-baada_ya_marekani_uk_nayo_yatahadharisha_shambulio_la_kigaidi_afrika_kusini
Serikali ya Uingereza imeitahadharisha Afrika Kusini juu ya uwezekano wa kujiri shambulio la kigaidi dhidi ya watalii wa kigeni nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 07, 2016 09:57 UTC
  • Baada ya Marekani, UK nayo yatahadharisha shambulio la kigaidi Afrika Kusini

Serikali ya Uingereza imeitahadharisha Afrika Kusini juu ya uwezekano wa kujiri shambulio la kigaidi dhidi ya watalii wa kigeni nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na London imesema kuwa, hatari ya kutokea shambulizi la kigaidi dhidi ya watalii wa kigeni katika maduka na maeneo ya starehe nchini humo, ipo juu sana. Aidha ripoti hiyo imedai kuwa maslahi ya raia wa Uingereza duniani yapo hatarini kutokana na makundi na watu walioathiriwa na mgogoro wa sasa nchini Iraq na Syria na kwamha, kuna haja ya kupewa umuhimu tahadhari hiyo. Tahadhari ya London inatolewa katika hali ambayo siku mbili zilizopita, ubalozi wa Marekani mjini Pretoria, ulionya juu ya uwezekano wa kutokea hujuma za kigaidi dhidi ya maeneo ya utalii nchini humo. Katika radiamali yake, serikali ya Afrika Kusini ilikadhibisha tahadhari hiyo na kuitaja kuwa isiyo na msingi wowote. Waziri wa Usalama nchini Afrika Kusini, David Mahlobo alisema kuwa, tahadhari ya kuwepo uwezekano wa kujiri hujuma ya kigaidi nchini humo haina msingi na kusisitiza kuwa, uwezo, uthabiti na demokrasia ya nchi hiyo vitaendelea kusalia mahala pake na kwamba hakuna anayeweza kutishia usalama wa nchi hiyo. Hadi sasa bado hakujatolewa sababu ya Marekani na Uingereza kuzungumzia vitisho hivyo tarajiwa dhidi ya taifa hilo la kusini mwa Afrika.