Majaji wa Afrika wawasili Kenya kufuatilia kesi ya uchaguzi wa rais
(last modified Mon, 29 Aug 2022 11:11:11 GMT )
Aug 29, 2022 11:11 UTC
  • Majaji wa Afrika wawasili Kenya kufuatilia kesi ya uchaguzi wa rais

Wanachama wa Jumuiya ya Majaji na Mahakimu wa Afrika wamewasili jijini Nairobi, kufuatilia shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) hivi karibuni.

Timu hiyo inaongozwa na Jaji Mkuu wa zamani wa Tanzania, Mohammed Chande Othman. Wengine katika timu hiyo ya uangalizi wa kesi hiyo ni Hakimu Lilian Tibatemwa-Ekirikubinza wa Mahakama ya Juu ya Uganda, Ivy Kamanga wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Malawi, Moses Chinhengo wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Lesotho, na Henry Mbha, Rais wa Mahakama ya Uchaguzi ya Afrika Kusini. 

Agosti 22, mgombea urais wa Kenya kwa tiketi ya chama cha Muungano wa Azimio la Umoja wa One Kenya, Raila Odinga aliwasilisha mahakamani shauri hilo, akisisitiza kuwa hakubaliani na matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa na IEBC, kwa sababu mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alikiuka katiba kabla ya kumtangaza mshindi.

Mwanasiasa huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 77  alisema makamishna wa tume hiyo hawakukubaliana kuhusu hesabu ya mwisho ya matokeo hayo yaliyompatia ushindi mshindani wake mkuu William Ruto, aliyewania kwa chama cha UDA.

Uchaguzi Kenya

Majaji saba wa Mahakama ya Juu ya Kenya wakiongozwa na Bi Martha Koome wanatazamiwa kuanza kusikiliza shauri hilo wiki hii na kutoa uamuzi ndani ya siku saba zijazo; na sasa mchuano mkali baina ya mawakili waandamizi wa upande wa Odinga, IEBC na timu ya Naibu Rais, William Ruto unatazamiwa kushuhidiwa mahakamani hapo. 

Makamishna wanne kati ya saba wa tume ya uchaguzi wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti, Juliana Cherera walijitenga na matokeo hayo yaliyotangazwa na Chebukati, wakidai kwamba marhala ya mwisho ya mchakato wa kuyatangaza haikuwa na uwazi. Mwenyekiti wa IEBC alimtangaza William Ruto mshindi wa uchaguzi wa rais, kwa kuapata kura milioni 7.1, sawa na asilimia 50.49 ya kura milioni 14 zilizopigwa, huku Raila akiambulia kura milioni 6.9, sawa na asilimia 48.85 ya kura.