Sep 09, 2022 12:26 UTC
  • Mahakama Angola yatupilia mbali kesi ya kupinga uchaguzi wa rais

Mahakama ya Katiba ya Angola imetupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa Agosti 24, yaliyompa ushindi mgombea wa chama tawala cha MPLA, Rais Joao Lourenco.

Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo jana Alkhamisi, ikipinga hoja zilizokuwepo kwenye shauri lililowasilishwa na Adalberto Costa Junior, kinara wa chama kikuu cha upinzani cha UNITA, aliyewania urais kwa chama hicho.

Uamuzi huo uliotolewa jana Alkhamisi ni wa mwisho na hauwezi kukatiwa rufaa, na sasa Rais Joao Lourenco anatazamiwa kuapishwa iki ijayo ili kuitawala nchi hiyo ya  kusini mwa Afrika yenye utajri wa mafuta kwa muhula wa pili.

Katibu Mkuu cha cha UNITA, Alvaro Chikwamanga Daniel alisema waliwasilisha kesi hiyo mahakamani kutaka kutupiliwa mbali tangazo la matokeo ya uchaguzi wa rais, kwani kulikuwepo na dosari nyingi katika uchaguzi huo.

Afisa huyo wa chama cha upinzani alisisitiza kuwa, chama hicho hakiyatambuia matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CNE) yanayoonesha kuwa, chama tawala kilipata asilimia 51.17 ya kura dhidi ya asilimia 43.95 ya mpinzani mkuu ambaye ni Costa Junior wa Chama cha Umoja wa Kitaifa wa Uhuru wa Jumla wa Angola (UNITA).

Rais Joao Lourenco. wa Angola kuongoza muhula wa pili

UNITA ilisisitiza kuwa, Tume ya Uchaguzi ilikataa kuyawianisha matokeo iliyoyasajili na yale yaliyosajiliwa na vyama vya siasa, na kwamba uchaguzi huo wa Agosti 24 uligubikwa na udanganyifu na uchakachuaji wa matokeo.

Viongozi wa UNITA wametoa mwito wa kufanyika maandamano ya amani ili kupinga matokeo ya Tume ya Uchaguzi na uamuzi wa Mahakama ya Katiba wa ubariki matokeo hayo. 

Tags