Oct 09, 2022 14:34 UTC
  • Wanajeshi 7 wa Djibouti wauawa katika shambulio la wabeba silaha

Askari saba wa jeshi la Djibouti wameuawa katika shambulio la genge moja la waasi wanaobeba silaha kaskazini mwa nchi.

Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Djibouti imesema, shambulio hilo lilifanyika juzi Ijumaa katika kambi ya kijeshi ya Garabtisan, kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Taarifa ya wizara hiyo imebainisha kuwa, hujuma hiyo imefanywa na kundi la wabeba silaha la Front for the Restoration and Democracy (FRUD). 

Wizara ya Ulinzi ya Djibouti imeongeza kuwa, "Licha ya wanajeshi wetu kupambana vikali, lakini shambulio hili limepekea wanajeshi wetu saba kuuawa, wanne wamejeuhiwa na sita wametoweka."

Kundi la FRUD ambalo akthari ya wapiganaji wake wanatoka katika jamii ya Afar ya kaskazini mwa nchi, lilianzisha uasi dhidi ya serikali mwaka 1991, wakidai kupigania maslahi ya jamii hiyo mkabala wa jamii nyingine yenye idadi kubwa ya watu ya Issas.

Wanajeshi wakilinda doria

Mashambulio ya aina hii ni nadra sana kuripotiwa nchini Djibouti, ambapo shambulio la mwisho kudaiwa kufanywa na kundi hilo ilikuwa Januari mwaka jana 2021.

Agosti mwaka jana, watu watatu waliuawa katika mapigano baina ya jamii hizo mbili katika mji mkuu wa nchi hiyo, Djibouti City.

Tags