Uganda yanakili kesi ya kwanza ya Ebola eneo la mashariki
Kesi ya ugonjwa wa Ebola imethibitishwa kutokea mjini Jinja kusini mwa Uganda, hiyo ikiwa ni kesi ya kwanza kuripotiwa katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Hayo yamesemwa leo Jumapili na Waziri wa Afya wa Uganda, Jane Ruth Aceng na kueleza kuwa, kesi hiyo iliyothibitishwa ni ya mwanaume wa miaka 45 ambaye aliaga dunia Alkhamisi.
Amesema wameanzisha uchunguzi wa kuwafuatilia watu waliotangamana na mhanga huyo wa maradhi hayo hatari ya kuambukiza. Hii ni mara ya kwanza kwa mripuko wa sasa wa Ebola kuenea nje ya kitovu cha maradhi hayo.
Haya yanajiri siku chache baada ya baraza la mawaziri la nchi hiyo kuchukua uamuzi wa kufunga skuli zote za awali, shule za msingi na shule za upili tarehe 25 mwezi huu wa Novemba kwa sababu madarasa yaliyojaa yanawafanya wanafunzi kuwa katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa Ebola.
Tangu ulipozuka ugonjwa huo katika wilaya ya Mubende Septemba 20 mwaka huu, ugonjwa wa Ebola umeenea katika maeneo mengi ya Uganda, ikiwa ni pamoja na katika mji mkuu, Kampala.
Takwimu za serikali zinaonesha kuwa, watu 135 wameambukizwa ugonjwa wa Ebola, ambapo 53 kati yao wamepoteza maisha kwa ugonjwa huo katika mripuko wa sasa.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Uganda imesajili zaidi ya kesi 150 zilizothibitishwa na zinazokisiwa kuwa ni za ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na vifo vya wagonjwa 64.