Dec 13, 2022 07:23 UTC
  • Jeshi la Nigeria latuhumiwa kuua watoto katika vita dhidi ya ugaidi

Jeshi la Nigeria linatuhumiwa kufanya mauaji makubwa dhidi ya watoto katika operesheni zake za kupambana na magenge ya kigaidi.

Askari 15 na raia zaidi ya 40 wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, maelfu kwa maelfu ya watoto wameuawa katika operesheni hizo za kuyakabili makundi ya kigaidi likiwemo la Boko Haram.

Mmoja wa wazazi ambao watoto wao wameuawa katika mashambulizi hayo ya wanajeshi wa Nigeria ameiambia Reuter kuwa, "Mimi nimepoteza watoto wangu pacha; wanajeshi walisema wamewaua wanangu hao eti kwa kuwa ni watoto wa Boko Haram."

Shuhuda mwningine aliyejitambulisha kwa jina la Falmata, amesema wajukuu zake watatu waliokuwa na miaka 9, 16 na 18 waliuawa katika shambulizi la jeshi la Nigeria.

Askari mmoja ambaye mwenzake aliuawa na magaidi kwa kupigwa risasi ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "Siwatazami kama watoto, nawaona tu kama Boko Haram, nikiwakamata, hata sitawapiga risasi, nitawachinja."

Boko Haram pia imekuwa ikiwaua na kuwateka nyara watoto wadogo

Hata hivyo Meja Jenerali Christopher Musa, kamanda anayeongoza operesheni dhidi ya ugaidi kaskazini mwa Nigeria amekanusha madai kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wanawalenga watoto katika mashambulizi hayo.

Amesisitiza kuwa, "Hayo hayajawahi kufanyika, hayafanyiki sasa wala hayatawahi kufanyika. Hiyo si hulka yetu, sisi ni wataalamu na pia wanadamu."

Tags