Ripoti: Eneo la Pembe ya Afrika linakabiliwa na ukame mbaya zaidi
(last modified Wed, 14 Dec 2022 07:51:29 GMT )
Dec 14, 2022 07:51 UTC
  • Ripoti: Eneo la Pembe ya Afrika linakabiliwa na ukame mbaya zaidi

Imeelezwa kuwa, eneo la Pembe ya Afrika linakabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa ya hivi karibuni.

Ripoti mbalimbali za mashirika ya misaada ya kibinadamu zinaonyesha kuwa, eneo la Pembe ya Afrika likiwemo la kaskazini mwa Somalia linakabiliwa na ukame mutlaki huku sehemu kubwa ya nchi hiyo ikitarajiwa kukumbwa na ukame pia katika miezi ya usoni.

Kufuatia baa hilo la ukame mkubwa, tawala za mataifa ya Pembe ya Afrika zimetangaza hali ya hatari.

Kutonyesha mvua na kukosekana maji kumewaathiri zaidi wafugaji katika eneo hilo huku wakulima nao wakishindwa kulima mashamba yao na hivyo kuweko tishio la kutokea baa la njaa.

Upatikanaji wa maji umekuwa wa shinda mno katika eneo la Pembe ya Afrika hukumu mifugo ikifa kutokana na kukosekana malisho

 

Ukame mbaya ambao haujawahi kushuhudiwa nchini Somalia na ambao unasababisha uhaba mkubwa wa chakula umepelekea maelfu ya raia wa nchi hiyo kukimbilia katiika nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya kutafuta msaada.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema kuwa, ukame wa muda mrefu nchini Somalia tayari umewakosesha makazi zaidi ya watu milioni moja.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza hivi karibuni kwamba sehemu kubwa ya eneo la Pembe ya Afrika linakabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 40 iliyopita. Watu wapatao milioni 46 wanakabiliwa na njaa kali katika eneo hilo.