Mar 12, 2023 07:31 UTC
  • Angola kutuma wanajeshi wake DRC kukabiliana na waasi wa M23

Angola imesema itatuma kikosi cha wanajeshi wake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, siku chache baada ya makubaliano ya kusitisha vita baina ya pande hasimu nchini humo kugonga mwamba.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais wa Angola Jumamosi imesema nchi hiyo itatuma askari mashariki mwa DRC, kwenda kuimarisha usalama katika maeneo yanayoshikilia na waasi wa M23, na pia kuwadhaminia usalama maafisa wanaotathmini usitishaji vita.

Taarifa hiyo hata hivyo haijaeleza idadi ya askari watakaotumwa, siku watakaotumwa na iwapo kitajiunga na kikosi cha kikanda kinachoundwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), au watakuwa sehemu ya askari wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO).

Wiki iliyopita, wanajeshi wapatao 100 wa Burundi waliwasili katika mji wa Goma mashariki mwa DRC ili kujiunga na kikosi cha kimataifa kinachosaidia Kinshasa kukabiliana na ongezeko la wanamgambo wenye silaha katika eneo hilo.

Waasi wa M23

Mapigano katika jimbo la Kivu Kaskazini yamesababisha idadi kubwa ya watu kuyakimbia makazi yao na kuzidisha mivutano ya kikanda, huku serikali ya DRC ikiishutumu Rwanda kwamba, inawaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo yanakanushwa vikali na serikali ya Kigali, ingawa yanaungwa mkono na madola ya Magharibi.

Huku hayo yakijiri, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limesema limesikitishwa sana na kuendelea mapigano makali kati ya makundi yasiyo ya wanamgambo yenye silaha na vikosi vya serikali yanayowafanya mamia kwa maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao Mashariki mwa nchi.

Tags