Angola, Misri kuishawishi UN kuziondolea vikwazo CAR na S/Kusini
(last modified Wed, 22 Jun 2016 04:04:42 GMT )
Jun 22, 2016 04:04 UTC
  • Angola, Misri kuishawishi UN kuziondolea vikwazo CAR na S/Kusini

Angola na Misri zimesema zitazishawishi nchi wanachama wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zikubali wazo la kuondolewa vikwazo Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini.

Georges Chikoti, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Angola amesema tayari Misri imetuma ujumbe wa ngazi za juu mjini Luanda kwa ajili ya kujadili kadhia hiyo. Amesema Angola kama mwenyekiti wa sasa wa Kongamano la Nchi za Eneo la Maziwa Makuu za Afrika itatumia nafasi yake hiyo kuzishawishi nchini zingine za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ziunge mkono azimio la kuziondolea vikwazo Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini. Nchi zingine wanachama wasio wa kudumu wa UNSC ni Japan, Malaysia, New Zealand, Senegal, Uhispania, Ukraine, Uruguay na Venezuela.

Haya yanajiri kufuatia kongamano la wiki iliyopita la nchi za Eneo la Maziwa Makuu za Afrika lililofanyika mjini Luanda Angola, ambapo viongozi wa nchi hizo 12 kwa kauli moja, waliutaka Umoja wa Mataifa kuiondolea vikwazo vya silaha Jamhuri ya Afrika ya Kati. Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia kwenye mapigano ya kikaumu tangu mwaka juzi.

Aidha viongozi hao waliitaka jamii ya kimataifa kuisaidia Sudan Kusini kujikusanya na kuzipa nguvu taasisi zake za uongozi sambamba na kuupatia ufumbuzi mzozo wa wakimbizi waliyoikimbia nchi na walioko katika kambi za wakimbizi ndani ya nchi. Hivi karibuni, Umoja wa Mataifa ulisema Sudan Kusini ipo katika ncha ya kuwekewa vikwazo vipya na jamii ya kimataifa kutokana na mwendo wa kinyonga wa kutekeleza makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka jana.