Saudi Arabia kufungua tena ubalozi wake huko Libya hivi karibuni
Ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia umeelekea Tripoli mji mkuu wa Libya kwa ajili ya kuchuguza taratibu za kufungua tena ubalozi wa nchi hiyo nchini Libya.
Ujumbe wa Saudi Arabia umekutana na kufanya mazungumzo na Rashid Abu Ghafeh, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Masuala ya Fedha ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya na Khalifa Al-Qaidi, Mkurugenzi wa Masuala ya Kiarabu katika wizara hiyo kuhusu uhusiano wa pande mbili na Saudia na hamu ya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ya kuimarisha uhusiano na kutimiza maslahi ya pamoja.
Mwezi Mei maka 2014 Saudi Arabia ilifunga ofisi zake za kibalozi nchini Libya kwa sababu ya hali ya usalama.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya miaka miwili iliyopita ilizitaka nchi zote kufungua tena balozi zao mjini Tripoli ili kuunga mkono mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo.
Libya bado inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa kutokana na kuwepo serikali mbili; moja ikiwa na makao yake mashariki mwa nchi ikiongozwa na Fatih Bashaga, na nyingine huko Tripoli chini ya uongozi wa Waziri, Mkuu Abdel Hamid al Dbeibeh. Serikali ya Al Dbeibeh inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa.