Jul 04, 2023 07:51 UTC
  • Waislamu Uganda na Nigeria walaani kuchomwa moto Qurani Tukufu Sweden

Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda (UMSC) limelaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden, huku uhalifu huo mkubwa wa kukichoma moto kitabu hicho kitakatifu katika nchi hiyo ya Magharibi ukiendelea kulaaniwa vikali na Waislamu kote duniani.

Naibu Mufti wa Uganda, Sheikh Muhammad Ali Waiswa ameiambia Iran Press katika ofisi za Baraza Kuu la Waislamu Uganda zilizopo mjini Kampala kwamba, "Kuchomwa moto Qurani huko Sweden ni kitendo cha kinyama na kilichopitwa na wakati, kama ambavyo kinawavunjia heshima Waislamu zaidi ya bilioni 2 kote duniani."

Naibu Mufti wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki ameitaka serikali ya Sweden na nchi nyingine za Ulaya kukoma kufanya vitendo vya aina hiyo vya kuzichochea na kuumiza hisia za Waislamu, na kuvuruga amani yao ya kijamii. 

Sheikh Ali Waiswa ameshangazwa na hatua ya serikali za Magharibi kutoa kibali, himaya na ulinzi wa kufanywa jinai kama hizo dhidi ya Waislamu. Amehoji kwa kusema, "Kwa nini ni haramu na jinai kupinga na kuandika kwa njia hasi juu ya Holocaust, lakini ni halali kuwadhalilisha Waislamu?"

Waislamu Nigeria wakiandamana kuitetea Qurani Tukufu

Huko magharibi mwa bara Afrika, Waislamu walikusanyika na kuandamana nchini Nigeria kulaani kitendo hicho cha kuvunjiwa heshima Qur'an tukufu nchini Sweden.

Maandamano hayo yaliyoongozwa na Harakati ya Kiislamu ya Nigeria yalifanyika katika mji wa Bauchi, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Kiafrika. Waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kukiheshimisha na kukienzi kitabu hicho kitukufu.

Juni 28, raia wa Sweden aliyejukana kwa jina la Salwan Momika (37) alichoma moto na kuchana nakala ya Qur'ani Tukufu huko Stockholm mji mkuu wa nchi hiyo katika siku ya kwanza ya Sikukuu ya Idul-Adh'ha.

 

Tags