Ulimwengu wa Spoti, Sep 1
Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu tuangazie baadhi ya matukio makubwa yaliyoripotiwa viwanjani ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa…..
Soka: Wanawake wa Iran watikisa Asia
Klabu ya Bam Khatoon FC ya Iran ilishinda timu ya Hong Kong ya Kitchee FC katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya AFC 2024/25 siku ya Jumamosi, na kuweka historia kwa kutinga hatua ya makundi. Akina dada hao wa Iran waliicharaza timu ya Hong Kong mabao 2-0 katika mchezo wa aina yake uliopigwa siku ya Jumamosi.
Timu hiyo wanawake ya Iran itamenyana na timu ya Melbourne City ya Australia, Chuo cha Wanazuoni wa Asia cha Thailand na Kaya–Iloilo ya Ufilipino katika hatua ya makundi, ambayo ni hatua hasasi ya mashindano hayo. Mashindano hayo ya kieneo yaliyong'oa nanga tarehe 25 Agosti, yatafikia ukingoni Mei 24 mwakani 2025.
Iran wang'ara karate Asia
Timu za vijana wa kike na kiume wa Iran zimeibuka kidedea katika mashindano ya karate ya Asia. Hii ni baada ya kushinda medali 6 za dhahabu, 1 za fedha na 4 za shaba katika siku ya mwisho ya Mashindano ya 2024 ya AKF Cadet, Vijana na Mabarobaro wenye chini ya miaka 21. Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la IRNA, Mashindano hayo ya Karate ya Asia yalifanyika Manila, mji mkuu wa Ufilipino, kuanzia Agosti 23 hadi 25 kwa kushirikisha makarateka 559 kutoka nchi 30, huku timu za vijana za Iran zilifanikiwa kusimama kwenye jukwaa la ubingwa.
Vijana wa Iran waliweza kupata medali 4 za dhahabu na 1 za shaba kwa upande wa wavulana na medali 2 za dhahabu, 1 ya fedha na 1 ya shaba kwa upande wa wasichana. Kwa jumla, wawakilishi wa Iran walishinda medali 10 za dhahabu, 4 za fedha na 9 za shaba na kupanda jukwani wakiwa washindi wa pili wa mashindano hayo ya Asia.
Kwengineko, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amempongeza Sareh Javanmardi kwa kuipatia nchi hiyo medali ya kwanza ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Paris 2024. Pezeshkian alituma ujumbe wake wa pongezi kwenye mtandao wa kijamii wa X Jumamosi usiku, saa chache baada ya Javanmardi kushinda dhahabu katika ulengaji shabaha kwa bastola kategoria ya P2-Women's Air Pistol 10m.
Rais alipongeza mafanikio mtawalia ya mwanariadha huyo wa kike, ambayo alisema ni matokeo ya bidii yake na dhamira kubwa aliyokuwa nayo. Javanmardi alimshinda mpinzani wake wa Uturuki katika fainali, na kupata alama 236.8 na kushinda medali ya kwanza ya dhahabu ya timu ya michezo wa Iran katika Michezo ya Walemavu ya mwaka huu. Wakati huo huo, mwanataekwondo wa Iran, Zahra Rahimi na warusha vitufe, Parastoo Habibi na Zafar Zaker wameshinda medali tatu za fedha tangu kuanza kwa michezo hiyo katika mji mkuu wa Ufaransa. Mashindano hayo ya Paralimpiki ya Paris yaliyoanza Agosti 28, yanatazamiwa kumalizika Septemba 3.
Soka Afrika
Baada ya kushindwa katika fainali mara mbili, timu ya kocha Birhanu Gizaw Heye, CBE Women FC imefanya vyema baada ya kuilaza Kenya Police Bullets 1-0 kwenye fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Abebe Bikila mjini Addis Ababa na kubeba Kombe la Mashindano ya Kandanda ya Kanda ya Afrika Mashariki na Kati Cecafa kwa upande wa Wanawake. Mfungaji bora wa shindano hilo Senaf Wakuma Zenaf Demise alifunga bao la pekee kunako dakika ya 79 baada ya timu yake kutawala mchezo kutoka mwanzo. Timu ya Kenya ambayo ilikuwa ikicheza fainali ya kwanza katika mchuano huo ilitumia mbinu ya kujilinda huku timu ya CBE ikizidisha shinikizo zaidi. Mwaka 2021 CBE ilipoteza katika fainali dhidi ya Vihiga Queens ya Kenya, na mwaka jana ilipokea kichapo kingine kutoka kwa JKT Queens ya Tanzania katika fainali iliyochezwa Uganda. Michuano hiyo ya kikaknda ilishirikisha timu nane kutoka Ethiopia, Uganda, Tanzania, Burundi, Djibouti, Sudan Kusini, Kenya na Rwanda.
Simba vs Al-Hilal
Klabu ya Simba ya Tanzania Jumapili ilishuka dimbani katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan katika uwanja wa KMC Complex Mwenge jijini Dar es Salaam. Mshambuliaji mpya wa Wekundu wa Msimbazi, Leonel Ateba alifunga bao lake la kwanza katika mechi hiyo. Simba ililazimishwa sare ya bao 1-1 na wageni. Katika mechi hiyo ya kimataifa ya kirafiki, Ateba alifunga bao hilo katika dakika ya 25 akimalizia pasi ya Shomari Kapombe. Hata hivyo bao hilo lilidumu kwa dakika 61 tu kwani Al Hilal walisawazisha katika dakika ya 86 kupitia kwa Serge Pokou. Al Hilal walilazimika kumaliza mechi wakiwa pungufu baada ya mchezaji wao, Suleiman Ezala kupewa kadi nyekundu dakika ya 55.
Kufunga bao kwa Ateba kunazidi kulipa matumaini benchi la ufundi la Simba katika kipindi hiki ambacho linajiandaa na mechi mbili za raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya. Septemba 13-15, Simba itaanzia ugenini Libya kisha kumalizia nyumbani mechi ya marudiano itakayopigwa kati ya Septemba 20 hadi 22.
Dondoo za Hapa na Pale
Klabu ya Chelsea inayoshiriki Ligi Kuu ya England ipo tayari kuchukua nafasi kubwa katika kukuza utalii Zanzibar ambapo Mabingwa hao mara mbili wa ligi ya Mabingwa Ulaya wanatarajiwa kuanzisha shule ya kukuza vipaji vya soka visiwani humo. Hayo yamebainishwa kufuatia kikao kati ya Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi na Mkuu wa Kitengo cha Mauzo ya Ubia wa Chelsea Barnes Hampel kilichofanyika Ikulu Mjini Zanzibar Alhamisi.
Ushirikiano huu kati ya Chelsea na Zanzibar unaashiria ushirikiano wenye matumaini ambao sio tu utaimarisha utalii bali pia utatoa fursa kwa maendeleo ya vijana kupitia vyuo vya soka.
Katika hatua nyingine, nyota wa kabumbu ya kimataifa, Victor Osimhen anaripotiwa kutathmini ofa nono kutoka kwa klabu ya Saudi Pro League Al-Ahli, ambayo inajumuisha mshahara wa kila mwaka wa (€ 30 milioni) zaidi ya pendekezo la Chelsea la zaidi ya (€ 10 milioni) kwa msimu. Kama ilivyoripotiwa na Sky Sports Italia, Al-Ahli imetoa ofa ya pili kwa fowadi huyo wa Nigeria, na mkutano kati ya wakala wa Osimhen, Roberto Calenda, na mkurugenzi wa michezo wa Al-Ahli unatarajiwa kujadili masharti hayo. Sky Sports Italiaimeripoti kuwa, Al-Ahli bado ina nia ya kupata saini ya Osimhen, ikitoa mkataba wa miaka minne wenye thamani ya Euro milioni 30 kwa mwaka. Di Marzio alitaja kuwa majadiliano kati ya kambi ya Osimhen na Al-Ahli yanatarajiwa kufanyika mjini Roma, yakiangazia dhamira ya klabu hiyo ya Saudia.
Na mshambuliaji wa Liverpool Mohamed Salah amesema kwa sasa analenga kucheza tu akifurahia kiwango chake huku akisubiri mkataba wake unaokaribia ukingoni utamatike ili azungumze kuhusu hali yake ya baadaye. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 alikubali mkataba mpya kuendelea kuchezea Liverpool, lakini utamalizika baada ya msimu huu wa 2024/2025. Septemba mwaka jana, Liverpool ilikataa kumuachilia ajiunge na Al-Ittihad baada ya klabu hiyo kuweka mezani kiasi cha Sh25.4 bilioni.