Oct 03, 2024 11:00 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrullah; Shahidi wa Njia ya Quds na Palestina

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel jioni ya Ijumaa (tarehe 6 Oktoba 2024) lilifanya mashambulizi ya kikatili ambayo hayajawahi kutokea katika viunga vya kusini mwa Beirut nchini Lebanon.

Katika mashambulizi hayo, ndege za kivita za Israel zilishambulia maeneo ya makazi ya raia huko Hareh ​​​​Harik katika viunga vya Beirut. Baada ya hapo, jeshi la utawala huo lilidai kwamba, shabaha ya mashambulizi haya ilikuwa kituo kikuu cha uongozi cha harakati ya Hizbullah. Mashambulizi hayo ambayo yalitekelezwa kwa ndege 8 za kivita za F-15 kwa kutumia mabomu ya kulipua mahandaki ya Marekani yenye uzito wa pauni 2,000 yalipekea kuuawa shahidi Sayyid wa Muqawama, na kiongozi wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah. Lakini swali linalojitokeza hapa ni kuwa, Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa nani?

Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa mmoja wa maulama wanamapambano na Mujahid wa zama hizi wa Lebanon na Katibu Mkuu wa tatu wa harakati ya Hizbullah ambaye alisimama kidete kupambana na uvamizi na jinai za utawala ghasibu wa Israel na kulitetea taifa madhulumu la Palestina. Alizaliwa tarehe 31 Agosti 1960 katika kitongoji maskini cha Carantina mashariki mwa Beirut. Baba yake, Sayyid Abdul Karim, na mama yake, Mahdia Safiyuddin, walihamia Beirut wakitokea katika kijiji cha "Al Bazourieh", huko Sur (Tyrus) kusini mwa Lebanon. 

Nasrullah alipata elimu ya msingi katika Shule ya Al-Najah huko Mashariki mwa Beirut, na sehemu ya elimu ya sekondari katika Shule ya Al-Tarbawiyah katika mtaa wa Kikristo wa Sinn al-Fīl. Baada ya kuanza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Lebanon mwezi Aprili 1975, alihamia katika kijiji cha Al Bazourieh, alikozaliwa baba yake, akiwa pamoja na familia yake, na kuendelea na elimu yake ya sekondari katika mji wa Sur (Tyrus).

Mwaka 1976, akiwa kijana mwenye umri wa miaka kumi na sita, na kwa kutiwa moyo na imamu wa Ijumaa wa mji wa Sur, ambaye alikuwa rafiki wa Sayyid Muhammad Baqir Sadr, faqihi na mwanafikra wa Kiislamu wa Iraq, alikwenda katika mji wa Najaf nchini Iraq kusoma sayansi ya kidini na kuanza masomo yake ya seminari katika mji huo. Sayyid Hassan alirejea Lebanon mwaka 1978 na kusoma katika Shule ya Imam al-Muntadhar, ambayo mmoja wa waanzilishi wake ni Shahidi Sayyid Abbas Mousawi; katibu mkuu wa pili wa harakati ya Hizbullah nchini Lebanon.

Sayyid Hassan Nasrullah

Sambamba na kuanza uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon na kukaliwa kwa mabavu maeneo ya kusini mwa nchi hiyo hapo 1982, Sayyid Hassan Nasrullah, akiwa pamoja na kundi la maulama wanamapambano waliasisi harakati ya mapambano ya Hizbullah kutoka ndani ya kundi la Amal, kutokana na ushawishi na msukumo wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Katika mwaka huo, Harakati ya Amal iligawanyika katika mikondo 2. Mkondo wa kwanza, ukiongozwa na Nabih Berri, ulitaka vikosi vya harakati hiyo kuwa karibu na National Salvation Front; na mkondo wa pili, ukiongozwa na Sayyid Abbas Mousawi na Sayyid Hassan Nasrullah, alitaka kulindwa vikosi vya wapiganaji wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia na kunolewa zaidi kwa ajili ya kukabiliana na uvamizi wa Israel.

Kuanzia 1982 hadi 1992, Sayyid Hassan alijikita katika shughuli zake ndani ya harakati ya Hizbullah. Mbali na kuwa katika Baraza Kuu la harakati hiyo, alihusika na maandalizi ya vikosi vya Muqawama na kuanzisha vitengo vya kijeshi. Alikuwa naibu wa Ibrahim Amin al-Sayyid (aliyesimamia Hizbullah huko Beirut) na naibu katibu mtendaji wa Hizbullah kwa muda. Mwakka 1992, baada ya kuuawa shahidi Sayyid Abbas Mousawi, Katibu Mkuu wa wakati huo wa Hizbullah, Sayid Hassan Nasrullah, ambaye wakati huo hakuwa na umri wa zaidi ya miaka 32, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa harakati hiyo kwa mwafaka wa wanachama wote wa baraza la uongozi la Hizbullah.

Kuuliwa shahidi Sayyid Abbas Mousawi pamoja na familia yake kulikuwa na taathira kubwa kwa watu wa Lebanon hasa wapiganaji wa Hizbullah, na baada ya hapo ndipo mapambano na mashambulizi ya Hizbullah yakachukua sura mpya chini ya uongozi na busara ya Sayyid Hassan Nasrullah, na uungaji mkono wa umma wa watu wa Lebanon kwa harakati hiyo ukaongezeka zaidi. Mwaka 1993 na 1996 utawala wa Israel ulitekeleza hujuma kkadhaa ikiwemo ile iliyopewa jina la "Operation Grapes of Wrath" ambazo zilikabiliwa na mapambano makali ya Hizbullah, licha ya kuwa na suhula ndogo zaidi za kijeshi. Baada ya hapo na polepole, Hizbullah ikawa jeshi lenye nguvu katika medani ya kukabiliana na uvamizi wa utawala wa Kizayuni.

Wapiganaji wa Hizbuullah

Tarehe 12 Septemba 1997, wapiganaji kakdhaa wa Hizbullah walivamia wanajeshi wa Israeli katika eneo la Jabal Al-Rafi'a kusini mwa Lebanon, na kuua wanajeshi wanne wa Iutawala huo ghasibu.. Walakini, wakati walipokuwa wakirudi kutoka kwenye operesheni hiyo wapiganaji hao walihusika katika mapigano makali na askari wengine wa Israel, na watatu kati yao waliuawa. Miili ya ya wawili kati yao iliangukia mikononi mwa askari wa Israel. Bila ya kujua utambulisho wa watu hao wawili, televisheni ya utawala wa Israel ilionyesha picha yao iliyokuwa imejaa damu, lakini ilifichuka haraka kuwa mmoja wa watu hao wawili ni Sayyid Hadi, mtoto wa Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah. Kuchapishwa kwa habari hiyo kulikuwa na sauti kubwa kama bomu katika jamii ya Lebanon ambayo ilisababisha mabadiliko muhimu sana. Katika siku ya kwanza ya kuuliwa shahidi mwanaye, Sayyid Hassan Nasrullah alisema yafuatayo katika shughuli ya kuwakumbuka mashahidi hao: "Sisi katika uongozi wa Hizbullah, tunasabilia watoto wetu kwa ajili ya Allah. Tunajisikia fahari wakati wana wetu wanapoenda mstari wa mbele wa vita na tunainua vichwa vyetu juu wanapoanguka kama kama mashahidi.”

Katika historia ya Lebanon, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe au katika mapambano ya kukabiliana na uvamizi wa kijeshi wa Israel, haijawahi kuonekana mtoto wa mmoja wa viongozi wa makundi ya kisiasa au ya wanamgambo akiuawa wakati wa mapambano. Tukio hili lilisababisha wimbi la hisia za huruma, heshima na kuvutiwa mno kwa watu wa dini na madhehebu tofauti za Lebanon na Katibu Mkuu wa Hizbullah, kwa namna ambayo watu wote wa taifa hilo waliathiriwa sana na tukio hilo. Viongozi wa kisiasa wa Lebanon pia walimtembelea Sayyid Nasrullah, mmoja baada ya mwingine, kutoa salamu za rambirambi kutokana na kuuliwa shahidi Sayyid Hadi na kusifu shakhsia adhimu, uaminifu na kujitolewa kwa Sayyid Nasrullah.

Sayyid Hassan Nasrullah akiuaga mwili wa mwanaye, Hadi Nasrullah

Mnamo mwaka wa 2000, wakati mazungumzo kati ya Yasser Arafat na maafisa wa Marekani na Israel ili kutatua mzozo katika eneo la Asia Magharibi yalipokwama na kugonga mwamba, jeshi la Israel lilijiondoa katika maeneo yaliyokuwa yakikaliwa kwa mabavu ya kusini mwa Lebanon katika hatua ya upande mmoja na bila ya kupata lolote kutoka upande wa Hizbullah. Majeshi la Israel yaliondoka katika maeneo yote yaliyokaliwa kwa mabavu, isipokuwa maeneo ya mpakani ya Mashamba ya Shab'a.

Kushindwa huku kwa fedheha, mbali na kuimarisha msimamo wa Hizbullah kama harakati ya Muqawama na mapambano, kulimfanya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah apate mafanikio yasiyo na kifani kati ya Waarabu na Waislamu kwa ujumla, na akatambuliwa kama mtu muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu. 

Kwa upande mwingine, kwa kuegemea kwenye mafanikio hayo, Hizbullah ya Lebanon iliweza kuimarisha uwepo wake katika uga wa kisiasa wa Lebanon, kwa kadiri kwamba, mbali na kushinda viti vingi vya Bunge, pia ilishika usukani wa idadi kadhaa ya wizara za serikali ya nchi hiyo. 

Ushindi mtawalia wa Hizbullah katika nyuga mbalimbali za kisiasa na kijeshi uliacha taathira kubwa miongoni mwa Wapalestina. Watu waliokimbia makazi yao wa Palestina, hususan vijana, ambao kwa miaka mingi walikuwa na matarajio makubwa kwa mchakato wa mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati, walitambua kwamba, tatizo la Palestina haliwezi kutatuliwa kwa mazungumzo na utawala vamizi na ghasibu, na kwa msingi huo, ilianzishwa Intifadha ya Pili ya Msikiti wa Al-Aqsa. Mapambano hayo ya Intifadha yaliipa Hamas nguvu mpya na kupiga hatua nyingine kwa ushindi wa harakati hiyo katika uchaguzi wa Bunge wa Palestina.

Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa katika orodha eti ya magaidi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa miaka mingi kutokana na vipigo alivyotoa kwa utawala huo katika kipindi cha uongozi wa harakati ya Muqawama ya Hizbullah hususan katika kipindi cha kuondoka utawala huo kwa madhila kusini mwa Lebanon na wakati wa vita vya  siku 33 za dhidi ya Wazayuni. Katika kipindi chote cha uongozi wake, Sayyid Nasrullah alinusurika majaribio kadhaa ya kuuawa na utawala wa kigaidi wa Israel, ikiwa ni pamoja na mwaka 2004, 2006 na 2011.

Hatimaye, Ijumaa ya tarehe 27 Septemba, kufuatia mashambulizi ya kinyama ya ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel katika viunga vya kusini mwa Beirut, jina la Sayyid Hassan Nasrullah lilijumuishwa katika orodha ya mashahidi wa Muqawama kama Sayyid Abbas Mousawi, Emad Mughniyeh, Kamanda Haj Qasim Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis na kubaki milele katika historia ya eneo la Magharibi mwa Asia na dunia nzima kwa ujumla.

Hizbullah ya Lebanon ilithibitisha kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, katika ujumbe rasmi uliotangazwa Jumamosi (Septemba 28), huku ikisema kuwa Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, amejiunga na msafara wa mashahidi wenzake wakubwa. Ilisema alipigana kwenye njia hiyo kwa karibu miaka thelathini, ikisisitiza kuwa: "Uongozi wa Hizbullah unafanya agano na shahidi huyo mkubwa, mtukufu na wa thamani kubwa kwamba, utaendeleza jihadi yake dhidi ya adui, kuitetea Gaza na Palestina na kuilinda Lebanon yenye nguvu na inayoheshimika.” Radhi za Allah ziwe juu yake....

Tags