Ulimwengu wa Spoti, Oktoba 28
(last modified Mon, 28 Oct 2024 09:44:16 GMT )
Oct 28, 2024 09:44 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Oktoba 28

Hujambo msikilizaji mpenzi na karibu tuangazie baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia....

Iran bingwa Handiboli Asia

Iran imeichakaza Thailand mabao 2-0 na kutwaa ubingwa wa Duru ya 3 ya Mashindano ya Handiboli ya Ufukweni kwa Vijana wa Asia. Iran ilifanikiwa kutinga fainali ya mashindano hayo ya kieneo baada ya kuzizaba Oman mabao 2-1, Jordan mabao 2-0, China mabao 2-1, na Qatar na Indonesia zote zikilambishwa mabao 2-0 katika mashindano hayo. Mashindano hayo ya 3 ya Mpira wa Mikono wa Ufukweni kwa Vijana wa Asia yalifanyika Bangkok, mji mkuu wa Thailand. Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa shindano hilo kufanyika nchini Thailand.

Kadhalika kwa ushindi huo, Jamhuri ya Kiislamu imefuzu kwa Mashindano ya Dunia ya Mpira wa Mikono ya Vijana ya 2025.

Nikudokeze pia kuwa, Iran itafungua Mashindano ya Mpira wa Mikono ya Wanawake wa Asia ya 2024 kwa mechi dhidi ya Japan.

Timu ya Melli Banovan itacheza na Japan mnamo Desemba 3 katika Kundi B. Waajemi pia watakutana na India na Hong Kong mnamo Desemba 4 na 6, mtawalia. Shindano hilo litakuwa ni toleo la 20 la Mashindano ya Handiboli kwa Wanawake wa Asia, ambayo yatafanyika kuanzia Desemba 1 hadi 12 huko New Delhi, mji mkuu wa India.

Mieleka U23: Iran bingwa

Timu ya mieleka ya Iran ya Greco-Roman imeshinda taji la Mashindano ya Dunia ya Vijana wenye chini ya miaka 23 ya 2024 huko Tirana, Albania. Jamhuri ya Kiislamu ilitwaa taji hilo Jumatano usiku ikiwa na pointi 149. Georgia ilifuatia kwa kushika nafasi ya pili kwa pointi 121 huku Armenia ikifunga orodha ya tatu bora kwa pointi 93. Iran ilijikusanyia medali tatu za dhahabu na nne za shaba katika mashindano hayo.

Timu ya mieleka ya Iran ya U23

Wakati huo huo, wanamieleka wa Iran Amirhossein Firouzpour na Amirreza Masoumi walishinda medali mbili za dhahabu katika mieleka mtindo wa kujiachia (Freestyle) kwenye Mashindano hayo ya Dunia ya U23.

Kabla ya hapo, Ebrahim Khari wa Iran alimshinda mwanamieleka wa Armenia, Levik Mikaleyan katika shindano la kuwania medali ya shaba kwa wanamieleka wenye kilo 61 na kuibuka kidedea.

AFC; Iran U17 yaendelea kung'aa

Iran imezidi kupiga muhuri tiketi yake ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Asia kwa vijana wenye chini ya miaka 17 Asia zitakazotifua mavumbi 2025. Hii ni baada ya kuigaragaza Jordan mabao 4-2 na kuhitimisha kampeni yao ya Kundi A ya kuwania kutinga fainali za AFC. Waarabu walianza mchezo kwa wasi wasi na kukanganyikiwa, kwani walijifunga la kisigino dakika 15 baada ya kuanza ngoma. Mabao mengine ya vijana hao wa Iran yalifungwa na Abolfazl Kazemi kunako dakika ya 71, Salman Ghafari (77), kiungo wa kati Mehrdad Agha Mohammadi (94, penati).

Kabla ya hapo, vijana hao wa Iran walivuna ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Syria katika mchezo mwingine wa Kundi A siku ya Ijumaa. Mshambuliaji Mahan Alipour alifunga bao la pekee la ushindi dakika ya 20 na kujipatia pointi. Huku Korea ikiwa tayari imeshika nafasi ya kwanza, matumaini ya Iran kusonga mbele yanategemea matokeo ya makundi yote 10, huku timu tano bora zilizoshika nafasi ya pili nazo zikifuzu kwa fainali.

Soka Afrika

Timu ya taifa ya soka ya Sudan usiku wa kuamkia Jumatatu hii imeitandika Taifa Stars ya Tanzania bao moja bila jibu katika mchezo wa Raundi ya Awali ya kuwania kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika. Bao la pekee na la ushindi la Sudan katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Cheikha Ould Boidiya jijini Nouakchoutt lilitiwa kimyani na mshambuliaji wa klabu ya al-Hilal, Muhammad Abdruhman al-Gharbal dakika ya 23 ya mchezo.

Kombe la Mataifa ya Afrika

Timu mbili hizo zitakutana katika mchezo wa marudiano mnamo Novemba 3 katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mshindi jumla atakutana na mshindi jumla wa mechi kati ya Ethiopia na Eritrea mwezi Disemba, ingawaje Tanzania na Kenya zimekwishafuzu kwa hisani ya tiketi ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya kibara.

Sudan na Tanzania zimekutana tena miezi 5 baada ya mechi ya kirafiki ambayo Tanzania ilishinda 1-0. Timu ya taifa ya kandanda ya Sudan inazidi kungaa, kwani katika mpambano dhidi ya Ghana katika awamu ya awali mnamo Oktoba 15 iliibuka kidedea.

Kwengineko, Shirikisho la Soka la Libya limeamriwa kulipa faini ya dola 50,000 baada ya kuitendea visivyo timu ya taifa ya Nigeria (Super Eagles) walipowasili nchini humo kwa ajili ya mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON 2025. Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limesema mchezo huo umefutwa, na timu ya Nigeria imepewa pointi zote tatu pamoja na mabao matatu. Nigeria ilisusia mechi hiyo baada ya kukwama uwanja wa ndege kwa zaidi ya saa 15 huku ikiilaumu Shirikisho la Soka la Libya kwa kutotuma magari ya kuwachukua hadi hotelini, ambapo ni umbali wa takriban saa 3.

Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika, CAF, linatarajia kufanya hafla za utoaji wa tuzo mbalimbali kwa vilabu na wachezaji wa Kiafrika Disemba 16, katika jiji la kitalii la Marrakech, nchini Morocco.

Hafla hiyo itahusisha ugawaji wa tuzo mbalimbali ikiwemo mchezaji bora wa Afrika anaecheza ligi za ndani, mchezaji bora Afrika anaecheza nje ya bara la Afrika, klabu bora ya mwaka ya Afrika pamoja na tuzo nyinginezo.

Berca yaionyoa Madrid

Na klabu ya Real Madrid imeburuzwa na kunyolewa bila maji na Barcelona katika ngoma ya mibabe iliyopigwa katika Uwanja wa Santiago Bernabue, na kufanikiwa kufuta uteja wa miaka kadhaa. Barca waliibuka na ushindi wa mabao 4 kwa 0 dhidi ya Madrid ambapo Robert Lewandoski alifanikiwa kucheka na nyavu mara mbili, huku kinda Lamine Yamal na Mbrazil Raphael Raphinha wakilizamisha kabisa jahazi la wenyeji.

Madrid yaondoka uwanjani kichwa chini

Kwa ushindi huo, Barca wanazidi kutuama kileleni mwa La Liga ikiwa na alama 30, pointi 6 zaidi ya mabingwa watetezi Madrid, baada ya mahasimu hao kucheza mechi 11 mpaka sasa.

………………..MWISHO……………

 

Tags