Ulimwengu wa Spoti, Feb 3
Mkusanyiko wa matukio makubwa ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, katika pembe mbali mbali za dunia….
Mieleka: Muirani aibuka wa 3 mashindano ya kimataifa
Mwanamieleka wa Iran Amir-Mohammad Yazdani ametwaa medali ya shaba katika kategoria ya wanamieleka wenye uzani wa kilo 74 katika Mashindano ya Kimataifa ya Mieleka nchini Russia.

Yazdani alipoteza mechi yake ya mwisho na kushika nafasi ya tatu katika kitengo chake, kwenye Mashindano ya Kombe la Ivan Yarygin la Russia yaliyofanyika huko Krasnoyarsk, Russia kuanzia Januari 23 hadi 26, na kuvutia wanamieleka nyota wakiwemo kutoka Russia na Bulgaria.
Tenisi: Kijana wa Iran aibuka wa 2 Kenya
Barobaro wa Iran aliibuka mshindi wa pili katika Mashindano ya Tenisi ya Dunia yaliyofanyika nchini Kenya. Kwa mujibu wa IRNA, mwakilishi huyo wa Iran, Ayrik Abedinzadeh alifikia nafasi ya pili katika kundi la vijana kwenye fainali za World Tennis Tour (G30) kwa kumlemea mwakilishi wa Macedonia.

Kijana huyo wa Kiirani alifanikiwa kuwabwaga washindani wake kutoka Kenya, Uhispania, Jamhuri ya Czech na Kazakhstan katika mashindano hayo ya kimataifa yaliyofanyika Nairobi, mji mkuu wa Kenya.
Ukweaji Barafu; Iran yang'ara Ufaransa
Raia wa Iran, Mohsen Beheshti Rad ameshinda medali ya fedha katika Mkondo wa Pili wa Kombe la Dunia la UIAA 2025 kwenye mchezo wa Kukweka Barafu huko Champagny-en-Vanoise kusini-mashariki mwa Ufaransa. Mmongolia, Mandakhbayar Chuluunbaatar alishinda dhahabu katika duru hiyo baada ya kuibuka kidedea. Medali ya shaba katika kitengo hicho ilinyakuliwa na mwanamichezo mwingine wa Kimongolia, Kherlen Nyamdoo.

Kabla ya hapo, Muirani Mohammadreza Safdarian aliibuka mshindi na kutwaa medali ya dhahabu katika mkondo wa kwanza wa fainali za Kombe la Dunia kwenye mchezo wa kukwea barafu, zilizofanyika huko Saas-Fee, nchini Uswisi, kuanzia Januari 23 hadi 25.
Riadha: Kenya yang'aa Japan
Mwanaridha anayeibukia kwa kasi kubwa wa Kenya, Alexander Mutiso Munyao ameendelea vyema na matayarisho ya kutetea taji lake la London Marathon baada ya kuibuka bingwa wa Kagawa Marugume Half Marathon nchini Japan siku ya Jumapili kwa rekodi mpya ya dakika 59 na sekunde 16. Bingwa huyo wa London Marathon 2024, ambaye amethibitisha kwenda kutetea taji hilo nchini Uingereza mwezi Aprili, alifuatiwa kwa karibu na Mkenya mwenzake Emmanuel Maru na Mjapan, Tomoki Ota.

Naye mwanadada Dolphine Omare Nyaboke kutoka Kenya alihifadhi umalkia wake kwenye mashindano hayo ya kilomita 21 kwa upande wa wanawake huko Japan. Nyaboke alishinda taji la kinadada kwa mwaka wa pili mfululizo akiimarisha rekodi yake ya Kagawa Marugume Half kutoka saa 1, dakika 06 na sekunde 07 hadi saa 1, dakika 06 na sekunde 05. Alimaliza mbele ya Muingereza Calli Hauger, Isobet Batt-Doyle wa Australia na Mkenya mwenzake Pauline Kamulu mtawalia. Katika hatua nyingine, Mkenya Vincent Kipchumba aliibuka mshindi wa Beppu-Oita Mainichi Marathon mjini Oita, huko huko Japan. Kipchumba alitwaa ubingwa kwa kutumia saa 2, dakika 06 na sekunde 01, mbele ya Wajapani Hiroki Wakabayashi na Shohei Otsuka. Hali kadhalika, siku ya Jumamosi, Alex Matata kutoka Kenya, aliibuka mshindi wa mbio za kilomita 21 za Ras Al Khaimah katika Umoja wa Falme za Kiarabu, baada ya kukata utepe kwa kutumia dakika 59 na sekunde 20. Alimaliza sekunde tano mbele ya Muethiopia Gemechu Dida huku Isaia Lasoi akifunga tatu-bora kwa dakika 59:26. Wakenya wanne, Judy Kemboi, Jesca Chelangat, Veronica Loleo na Brillian Jepkorir, walikamilisha ndani ya 10-bora katika safu ya wanawake katika nafasi za pili, tatu, saba na tisa, mtawalia. Muithiopia Ejgayehu Taye, aliyekuwa ametangaza atavizia rekodi ya dunia ya Mhabeshi mwenzake Letesenbet Gidey ya saa 1, dakika 2 na sekunde 52, alitwaa taji kwa kutumia saa 1, dakika 05 na sekunde 52.
Kwingineko, mshindi wa zamani wa nishani ya shaba wa Riadha za Dunia za Ukumbini mbio za mita 800, Noah Kibet aliridhika na nafasi ya tatu katika mbio za Meeting Miramas Metropole nchini Ufaransa, siku ya Ijumaa. Kibet aliyepigiwa upatu kutawala mbio hizo, aliandikisha dakika 1, sekunde 46.05, nyuma ya Mmorocco Abdelati El Guesse na Mfaransa Yanis Meziane.
Soka Afrika; Tanzania tayari kwa CHAN, AFCON
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema serikali imejipanga vyema kukamilisha maandalizi yote muhimu ikiwemo miundombinu kwa ajili ya Michuano ya Mpira wa Miguu kwa Nchi za Africa CHAN na AFCON. Ameyasema hayo Jumamosi ya Februari Mosi jijini Dodoma na kuongeza kuwa, tayari ukaguzi wa baadhi ya viwanja umefanyika na vimeonekana kukidhi vigezo.

Michuano ya AFCON 2025, itakayofanyika kuanzia tarehe 21 Desemba hadi 18 Januari 2026, itachezwa katika miji sita ya Morocco na viwanja tisa tofauti. Timu zimepangwa katika makundi sita, kila kundi likiwa na timu nne. Kundi A: Morocco, Mali, Zambia, na Comoro. Kundi B: Misri, Afrika Kusini, Angola, na Zimbabwe. Kundi C: Nigeria, Tunisia, Uganda, na Tanzania, huku Kundi D: Senegal, DR Congo, Benin, na Botswana. Kundi E: Algeria, Burkina Faso, Guinea ya Ikweta, na Sudan, huku Kundi F: Ivory Coast, Cameroon, Gabon, na Msumbiji.
Dondoo za Hapa na Pale
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imezitaka klabu za soka barani Ulaya zinazopata ufadhili kutoka Rwanda kuvunja ushirikiano na Kigali, ikidai kuwa serikali ya Rais Paul Kagame inazifadhili 'Fedha zilizolowa damu,' kutokana na mgogoro unaoendelea mashariki mwa DRC. Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Therese Kayikwamba Wagner ameziandikia klabu za Arsenal ya Uingereza, PSG ya Ufaransa na Bayern Munich ya Ujerumani kusitisha ushirikiano wao wa ufadhili wa mauzo chini ya mpango wa, 'Visit Rwanda,' wakidai kwamba idadi kubwa ya wanajeshi wa Rwanda wanapigana na jeshi la serikali huko Goma wakisaidiana na kundi la waasi la M23.

Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu zaidi 700 na kujeruhi 2,800 katika muda wa siku tano.
Na katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, klabu ya Arsenal siku ya Jumapili iliwanyoa bila maji mabingwa watetezi Manchester City kwa kuwagaragaza mabao 5-1 wakiupigia nyumbani Emirates. Mashabiki wa Manchester United waliamua kuwatia shime watani wao wa City baada ya kupoteza kwa mabao 2-0 walipovaana na Crystal Palace. Hata hivyo matumaini yao yalizimwa na mabao ya Martin Odegaard, Thomas Partey, Myles Lewis-Skelly, Kai Havertz na Ethan Nwaneri.

Wabeba Bunduki sasa wamekamilisha mechi 14 bila kupoteza kwenye Ligi ya EPL. Ushindi huo wa kishindo wa Jumapili unafikisha alama za vijana hao wa Mikel Arteta kuwa 50 kutokana na mechi 24. Wapo katika nafasi ya pili wakiwa na alama sita nyuma ya vigogo Liverpool walio na mechi moja ya akiba. Nottingham Forest kwa sasa wametulia katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 47.
Na nyota wa Manchester United Marcus Rashford, amekata shauri na kuamua kujiunga na Aston Villa kwa mkataba wa mkopo. Mshambuliaji huyo hajawa na uhusiano mzuri na kocha mpya wa Mashetani Wekundu, Ruben Amorim, tangu atue Old Trafford. Inaelezwa kuwa, mshambuliaji huyo anatarajiwa kuendelea kupokea mshahara wake wa pauni 350,000 kwa wiki, na mkataba wake na United unatarajiwa kumalizika Juni 2028.

Taarifa inasema kuwa, Villa watalipa asilimia 70 ya mshahara huo, huku mambo mengine yakiwa makubaliano yao na Man United. Rashford amefanikiwa kufunga mabao 138 akiwa na United baada ya kucheza michezo 426.
……………….TAMATI……..……..