Ulimwengu wa Spoti, Feb 17
Hujambo mpenzi na ashiki wa spoti, natumai u mzima wa afya. Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyoshuhudiwa ndani ya siku zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa.
Futsal: Mabanati wa Iran bingwa wa Asia
Timu ya mpira wa miguu unaochezewa ukumbini ya Iran imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Wanawake ya Futsal ya 2025 ya Shirikisho la Futsal Asia CAF. Hii ni baada ya kuibaiza Tajikistan mabao 10-1 katika ngoma ya fainali iliyopigwa Jumapili huko Dushanbe, mji mkuu wa Tajikistan. Mabao ya Iran yalifungwa na Maral Torkman (mabao mawili), Fereshteh Karimi (mabao mawili), na Roghayeh Soume'eh. Wengine waliofanikiwa kucheka na nyavu ni Nasimeh Gholami, Mahtab Banaei, Zahra Kianimanesh, Fatemeh Hosseini, na Mahsa Alimadadi na kuipa ushindi timu hiyo ya wanawake wa Iran kwenye mchuano huo. Iran ilitinga fainali baada ya kuisasambua Uzbekistan mabao 9-0, Kyrgyzstan mabao 10-0, na Turkmenistan mabao 5-1.

Ushindi huo wa Jumapili unaifanya Iran kutwaa mataji yote manne katika duru nne za mashindano hayo tangu yaliyopoanzishwa. Michuano hiyo ya kibara, iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka la Asia ya Kati (CAFA), ilifanyika Dushanbe kuanzia mnamo Februari 9 hadi 16.
Soka; Iran yaitandika Yemen Kombe la Asia
Timu ya mabarobaro ya Iran imefuzu katika hatua ya mtoano ya Mashindano ya Soka ya AFC ya Asian Cup China 2025 kwa vijana wenye chini ya miaka 20, baada ya kuipepeta Yemen mabao 6-0 katika mechi ya Kundi C iliyochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Mafunzo ya Vijana wa Shenzhen, kusini mashariki mwa China. Iran ilicheza kwa kasi kuanzia mwanzo hadi mwisho, huku Abolfazl Zamani akicheka na nyavu mara mbili na kuihakikishia timu hiyo ya Asia ya Kati inasonga mbele. Kusonga mbele kwa vijana wa Iran pia kulichangiwa na Indonesia kushindwa kuifunga Uzbekistan katika mchezo mwingine Jumapili, ambapo ilikubali kulimwa mabao 3-1. Mbali na Abolfazl Zamani, mabao mengine ya Iran kwenye mechi hiyo yalifungwa na Yaghoob Barajeh, Esmaeil Gholizadeh Mohammed Moqbel, na Abolfazl Zoleikhaei.
Soka: Michuano ya Kombe la Hazfi (Mtoano) yachacha
Kwengineko, Michuano ya Kombe la Hazfi la Iran imeendelea kutifua mavumbi, huku baadhi ya miamba ya soka hapa nchini ikibanduliwa, na wengine wakisogea mbele kwa mbide kwenye mtoano huo. Timu ya kandanda ya Esteghlal siku ya Alkhamisi iliichabanga Shams Azar mbao 2-1 na kujikatia tiketi ya kufuzu kwa robo fainali ya Kombe la Hazfi la Iran 2024/25. Mohammadreza Azadi aliwaweke wageni kifua mbele katika dakika ya 27, lakini Ahmadreza Zendehrouh alisawazisha bao hilo katika muda wa majeruhi.

Ramin Rezaeian aliyetumia mguu wa kushoto alifunga bao la ushindi la The Blues wa Tehran kunako dakika ya 95 kwenye mchuano huo uliopigwa katika Uwanja wa Sardar Azadegan mjini Qazvin.
Katika pambano jingine la kusisimua, Sepahan iliilaza chali Persepolis kwa kuitandika mabao 3-2 katika mechi ya Raundi ya 16 ya Kombe la Hazfi siku ya Jumatano. Mechi hiyo ilipigwa katika Uwanja wa Naghsh-e Jahan mjini Isfahan. Kiungo wa Sepahan, Aboubakar Kamara alipigwa kadi ya pili ya njano katika dakika ya 102, na hivyo kuifanya timu hiyo kuwa wachezaji 10. Pamoja na hayo, lakini Wekundu wa Tehran hawakuweza kutumia vizuri fursa hiyo ya idadi, kwani washambuliaji wao hawakuweza kuona wavu. Mbali na hayo, Mes walipoteza kwa kuzabwa na Nassaji bao 1-0 mjini Rafsanjan, klabu ya daraja la kwanza Paykan walitoka nyuma na kuishinda Foolad kwa mabao 3-2 mjini Tehran, wakati ambapo Sanat Naft walikuwa wakiilaza Be'sat Kermanshah mabao 2-0 mjini Abadan. Hali kadhalika, timu za kandanda za Malavan na Gol Gohar zilijikatia tiketi ya kufuzu hatua robo fainali ya Kombe la Hazfi la Iran la 2024/25 siku ya Ijumaa. Kombe la Hazfi ni mashindano ya mtoano ya Iran ambayo huandaliwa kila mwaka na Shirikisho la Soka la Iran. Sepahan ndio mabingwa watetezi wa michuano hii ya aina yake.
Israel yalishwa kadi nyekundu mechi ya Madrid
Mashabiki wa klabu ya Osasuna ya Uhispania wametoa wito wa kukomeshwa uhalifu wa utawala wa Israel huko Palestina katika mechi na mpira wa miguu iliyofanyika Jumamosi kati ya timu hiyo dhidi ya Real Madrid. Mashabiki wa Osasuna waliinua bango lenye maandishi: "Ionyeshe Israel Kadi Nyekundu" wakati wa mechi ya soka ya timu hiyo dhidi ya Madrid. Shirika la Habari la Iran (IRNA) limeripoti kuwa, idadi kubwa ya mashabiki wa soka pia walifika kwenye uwanja huo wakiwa na bendera za Palestina. Kundi hilo la mashabiki pia lilisambaza vipeperushi vya kuwahimiza mashambiki wenzao kushikilia karatasi nyekundu na kutaka Israel ipigwe marufuku kushiriki katika michezo ya soka ya kimataifa. Real Madrid ililazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Osasuna katika mechi ya ugenini ya La Liga ya Uhispania Jumamosi na kujiweka katika hatari ya kupoteza nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi ya Soka la Uhispania.

Wiki iliyopita mashabiki wa timu ya Celtic ya Scotland pia waliendelea kulaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Palestina na Lebanon katika mechi ya mkondo wa kwanza ya hatua ya mtoano ya UEFA Champions League dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani iliyochezwa Jumatano ya Februari 12. Mashabiki wa timu ya Celtic, maarufu kama Green Brigade waliongoza maandamano makubwa wakiwa na bango lililosema "Show Israel The Red Card," likizitaka UEFA na FIFA kuchukua hatua dhidi ya Israel katika mashindano hayo. Kundi la mashabiki hao lilisambaza vipeperushi vinavyowahimiza mashabiki kuinua juu karatasi nyekundu zinazotoa wito wa kufukuzwa Israel katika mashindano ya soka ya Ulaya na katika ngazi za kimataifa kutokana na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Palestina.
Rwanda vs DRC michezoni
Na Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo imelitaka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Kikapu la NBA kufuta mikataba ya udhamini na Kigali, kutokana na kile walichokitaja kuwa ukaliaji wa mabavu unaofanywa na wanajeshi wa Rwanda mashariki ya DRC. Mwito huo wa DRC unakuja baada ya maombi kama hayo kuwasilishwa na Kinshasa kwa usimamizi wa mashindano ya magari ya langalanga ya Formula One, ambao uko kwenye mazungumzo na Rwanda juu ya kuandaa mashindano makubwa ya dunia. Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Therese Kayikwamba Wagner ameiambia NBA kuwa, kwa kushirikiana na Rwanda, itakuwa inaunga mkono kwa njia isiyo ya moja kwa moja mauaji na jinai zinazofanywa na waasi wa M23 mashariki mwa Kongo DR, wanamgambo ambao wanadaiwa kuungwa mkono na serikali ya Kigali. Kabla ya hapo, Wagner aliziandikia barua klabu za Arsenal ya Uingereza, Paris Saint-Germain ya Ufaransa na Bayern Munich ya Ujerumani kusitisha ushirikiano wao wa ufadhili wa mauzo chini ya mpango wa, 'Visit Rwanda,' wakidai kwamba idadi kubwa ya wanajeshi wa Rwanda wanapigana na jeshi la FARDC huko Goma wakisaidiana na kundi la waasi la M23.

Waziri Wagner amesema kwamba, 'Rwanda inastahili kulaumiwa kwa hatua zake ndani ya DRC kwani Umoja wa Mataifa umeripoti kwamba kikosi cha wanajeshi 4,000 kutoka Rwanda kiko ndani ya DRC na kinashikriki kwenye vita vinavyoendelea nchini humo.' Mwanadiplomasia huyo wa Kongo ameiambia Sky News kwamba, kuna haja kwa hatua kuchukuliwa na timu hizo za soka dhidi ya Rwanda, kwa kuwa DRC, ina maelfu pia ya mashabiki wa klabu hizo za kandanda.
…………………TAMATI…………….