Ulimwengu wa Spoti, Feb 24
Hujambo msikilizaji mpenzi na hasa mfuatiliaji wa matukio ya spoti. Karibu tuangazie baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyoshuhudiwa ndani ya siku zilizopita katika kona mbali mbali za dunia.....
Ligi ya Mabingwa Asia: Teraktor yasonga mbele
Klabu ya Teraktor ya Iran imefanikiwa japo kwa mbinde kutinga hatua ya robofainali ya Ligi ya Mabingwa ya Asia ya Shirikisho la Soka barani hapa AFC. Hii ni baada ya kuambulia sare ya kufungana mabao 3-3 na klabu ya Al-Khaldiya ya Bahrain katika kitimutimu cha mkondo wa pili wa Raundi ya 16.

Watengeneza matrekta wa Iran wamesogea mbele kwa kuifunga klabu hiyo ya Bahrain jumla ya mabao 5-4. Wakati huo huo, klabu nyingine ya soka ya Iran ya Esteghlal ilivuna ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Al Rayyan ya Qatar na kusogea mbele kwa madaha kwenye michuano hiyo ya kibara ya AFC Champions League Elite kwa msimu wa 2024/25. Mabao ya Wanasamawati hao wa Tehran katika ngoma hiyo ya Jumanne yalitiwa kimyani na Mohammadreza Azadi na Alireza Kooshki. Ushindi huo wa Esteghlal umewafanya wamalize mkondo huo katika nafasi ya sita kwa pointi tisa, wakibebewa na Al Rayyan jedwalini.

Matokeo hayo pia yaliisukumiza Persepolis katika nafasi ya tisa, na hivyo kubanduliwa nje ya ligi hiyo ya miamba ya soka barani Asia.
Kombe la Asia-U20; Iran yazimwa
Timu ya soka ya mabarobaro wa Iran imendolewa kiume kwenye Kombe la Asia kwa vijana wenye chini ya miaka 20. Hii ni baada ya kuzabwa mabao 4-3 kwenye upigaji matatu, kufuatia sare ya bao 1-1 katika mechi ya robo fainali ya AFC U20 Asian Cup China Jumapili dhidi ya Japan. Mechi hiyo ilipigwa katika Uwanja wa Mafunzo ya Soka ya Vijana wa Shenzhen. Kabla ya hapo, Iran iliichabanga Uzbekistan mabao 2-1 katika mechi ya mwisho ya Kundi C mnamo Jumatano.

Wakati huo huo, timu ya kandanda ya Iran ya vijana wenye chini ya miaka 17 ilikubali kichapo cha mabao 4-1 kutoka Tajikistan kwenye upigaji matuta, na kuvuta mkia kwenye Kombe la Maendeleo-2025 mnamo Ijumaa. Iran inayonolewa na Abbas Chamanian ilishindwa kufurukuta mbele ya Kazakhstan, Azerbaijan, Russia na Tajikistan katika michuano hiyo ya kikanda. Mashindano hayo yalifanyika mjini Minsk, Belarus kuanzia Februari 15 hadi 21.
Kikapu: Iran yailemea India
Ni rasmi sasa kwamba timu ya mpira wa kikapu ya Iran imetinga mzima mzima michuano ya Kombe la Basketboli la Asia ya FIBA 2025, baada ya kuikandamiza India kwa vikapu 106-55 kwenye Ukumbi wa Mpira wa Kikapu wa Azadi hapa Tehran, siku ya Ijumaa. Wakiwa na raghba ya kutamba baada ya kupigwa breki na Qatar mnamo Novemba mwaka jana, timu hiyo ya taifa ya Iran iliegemea kwenye safu ya ulinzi ili kurekebisha makosa ya nyuma, katika hatua ya robo ya pili ambayo wageni hawakuweza kupona. Mohammad Amini aliibuka kidedea kwa ushindi huo akiwa na pointi 33 katika moja ya maonyesho ya kuvutia ya mtu binafsi ya Kufuzu kwa Kombe la Asia.
Riadha: Mtanzania awika Korea
Mwanariadha nyota wa Tanzania, Gabriel Geay ameibuka kidedea katika mbio za Daegu Marathon 2025 zilizofanyika Jumapili huko Korea Kusini. Katika mbio hizo za Jumapili, Geay ambaye ni mshindi wa pili wa Boston Marathon 2023, alimshinda bingwa wa Ethiopia aliyeng’ara Dubai Marathon 2024, Addisu Gobena kwa kutumia muda wa saa 2, dakika 5 nasekunde 20.

Nafasi ya tatu imetwaliwa na Mhabeshi mwingine, Dejene Magersa aliyetumia muda wa saa 2:05:59. Mbio za Daegu Marathon zinakuwa mashindano ya pili mwaka huu kwa Geay kushiriki baada ya kukutana na changamoto za kiafya mwaka 2024, ikiwamo kuchemsha katika Olimpiki 2024. Mbio za kwanza kwake kushiriki mwaka huu zilikuwa ni za Aramco Huston Half Marathon ambazo zilifanyika Marekani na kufanikiwa kumaliza wa tatu kwa dakika 59:18.
Kwa upande wa wanawake, Meseret Balete wa Ethiopia alitamalaki mbio hizo za Korea Kusini na kumaliza wa kwanza kwa muda wa saa 2 dakika 24na sekunde 08 huku mshindi wa medali ya dhahabu ya Olimpiki ya Rio De Janeiro 2016, Ruth Jebet wa Bahrain mzawa wa Kenya, akimaliza wa pili kwa zaidi ya dakika moja na nusu. Mbio hizo pia zilishuhudiwa Tigist Girma wa Ethiopia akimaliza nyuma ya Ruth zaidi ya dakika moja baadaye. Tofauti na mbio nyingine, katika mbio hizo za Korea Kusini, wanariadha wa Kenya wakigaragazwa vibaya ambapo kwa upande wa wanaume, Gilbert Kibet aliyepigiwa upatu kung'ara, alimaliza wa sita na kufuatiwa na mwenzake Stephen Kiprop. Kwa upande wa wanariadha wa kike wa Kenya, Vivian Jerotich alimaliza nafasi ya tano.
Dondoo za Hapa na Pale
Rais wa Shirikisho la Soka nchini Cameroon, Samuel Eto'o ameshinda kesi yake dhidi ya Shirikisho la Soka Barani Afrika [CAF], iliyomzuia kuwania nafasi ya ujumbe kwenye Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo. Hata hivyo Rais huyo wa Fecafoot alitozwa faini ya dola 200,000 za Marekani, kwa kosa la kuvunja na kukiuka kanuni za Shirikisho la Soka Barani Afrika. Uchaguzi wa Rais na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF unatarajiwa kufanyika mwezi ujao Machi.

Mbali na hayo, aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Uhispania, Luis Rubiales amepatikana na hatia ya kumnyanyasa kimapenzi mchezaji wa timu ya taifa ya Uhispania, Jenni Hermoso, baada ya kumpiga busu mdomoni bila idhini yake wakati timu hiyo iliposhinda Kombe la Dunia 2023. Rubiales, 47, pia ameamrishwa na mahakama kutomkaribia Hermoso, 34, wala kuwasiliana naye kwa kipindi cha mwaka mmoja. Isitoshe, Rubiales amepigwa faini ya Yuro 10,000. Aliponea adhabu kwa kosa jingine la madai ya kujaribu kumshinikiza Hermoso aseme kuwa alimpa ruhusa ampige busu wakati huo wa fainali za Kombe la Dunia la Wanawake.
Na katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, vinara Liverpool wamejiweka pazuri zaidi kutwaa ligi baada ya kuwasasambua mabingwa watetezi Manchester City Jumapili. Liverpool wamefungua mwanya wa alama 11 juu jedwalini, kupitia mabao ya kipindi cha kwanza kutoka kwa nyota Mohamed Salah na Dominik Szoboszlai katika Uwanja wa Etihad. Vijana wa kocha Arne Slot hawajapoteza mechi ya ligi kwa mara ya 14 mfululizo, tangu walimwe bao 1-0 na Crystal Palace mwezi Aprili mwaka jana 2024. Reds pia waliimarisha rekodi yao ya kuwapepeta mabingwa watetezi nyumbani na ugenini hadi mechi saba.

Katika mechi nyingine Jumapili, Newcastle waliifyeka Nottingham Forest mabao 4-3, ambapo mabao mawili yalifungwa na Alexander Isak ikiwemo penalti, huku Lewis Miley na Jacob Murphy wakicheka na nyavu mara moja kila mmoja. Nambari mbili Arsenal wenye alama 53 kwa sasa, walipata pigo baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 mikononi mwa West Ham, Jumamosi, wakati ambapo watani wao Manchester United nao walikuwa wanalazimishwa sare ya mabao 2-2 na Everton.
……………………..MWISHO…………….