Ulimwengu wa Spoti, Machi 10
Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa......
Kabaddi ya Wanawake Asia; Iran yaibuka ya 2
Timu ya taifa ya Kabaddi ya Iran imeibuka mshindi wa pili baada ya kushindwa katika mechi ya fainali ya Mashindano ya 6 ya Kabaddi ya Wanawake wa Asia siku ya Jumamosi. Iran ilishindwa kufurukuta mbele ya Wahindi kwenye kitimutimu hicho cha fainali na kukubali kichapo cha 32-25. Timu ya Kabaddi ya wanawake ya Iran ilitinga fainali kwa ushindi wa kishindo wa 41-18 dhidi ya Bangladesh. Michuano hiyo ya kibara ya mchezo wa Kabbadi ilifanyika hapa Tehran huku timu saba zikishiriki.

Huku hayo yakiarifiwa, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Mohammadreza Aref ameipongeza Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Walemavu ya Iran (NPC) kwa kushinda Tuzo ya Kutambuliwa kwenye Siku ya Kimataifa ya Wanawake ya 2025. Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki ya Walemavu (IPC) ilitangaza washindi watatu wa kipekee ikiwemo Iran, wa Tuzo za Kifakhari za Siku ya Kimataifa ya Wanawake iliyoadhimishwa Machi 8.
Mieleka: Iran yang'ara Albania
Shirikisho la Mieleka Duniani (UWW) limetangaza matokeo ya mashindano ya viwango nchini Albania, ambapo wanamieleka wanne wa Iran ni kati ya wanamieleka bora katika kategoria za Freestyle na Greco-Roman. Kufuatia mashindano ya pili ya viwango vya Freestyle na mieleka ya Greco-Roman huko Albania, ambayo yalifanyika kutoka Februari 26 hadi Machi 2, UWW ilitangaza washindani wakuu katika kategoria mbalimbali za uzani.

Wanamieleka wa Iran, Rahman Amouzad Khalili na Amir-Hossein Zare, walioshinda medali za dhahabu katika kitengo cha kilo 65 na kilo 125, waliongoza katika vitengo hivyo. Katika mieleka ya Greco-Roman, Saeed Esmaeili na Mohammad-Hadi Saaravi waliibuka wa kwanza katika makundi ya kilo 67 na kilo 97, mtawalia. Amin Mirzazadeh, Ali-Reza Mohmadi, Mohammad-Ali Gerayi, na Pooya Dadmarz walipata nafasi ya pili katika kategoria tofauti za Greco-Roman. Katika mashindano ya mitindo huru, Hassan Yazdani na Kamran Ghasempour walishika nafasi ya pili na tatu katika kategoria za kilo 86 na kilo 92, mtawalia.
Futsal: Iran mshindi wa 2 Copa Intecontinental
Timu ya taifa ya futsal ya Iran ilishindwa kwa mabao 3-0 na Brazil na kumaliza mshindi wa pili katika michuano ya Copa Intercontinental de Seleções siku ya Jumapili. Mabao ya mwenyeji Brazil yalifungwa na Felipe Valério na Neguinho (mabao mawili) kwenye fainali hiyo iliyopigwa Jumapili. Afghanistan iliibuka ya tatu baada ya kuifunga Greenland mabao 6-4.

Awali Iran ilikuwa imepoteza kwa magoli 5-2 ilipovaana na Brazil katika michuano hiyo ya mabara, lakini ikaishinda Greenland kwa mabao 11-2 na Afghanistan magoli 4-3. Mashindano hayo yalifanyika kuanzia Machi 5 hadi 9 katika Ukumbi wa Ginasio De Esportes e Lazer Max Rosenmann huko Sao Jose dos Pinhais (Jimbo la Parana) nchini Brazil.
Kenya bingwa Raga ya Wanawake Afrika
Timu ya taifa ya raga ya wanawake ya Kenya (Kenya Lionesses) wameibuka kidedea kwenye mashindano ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Challenger Series, baada ya kumsagasaga vibaya mwenyeji Afrika Kusini siku ya Jumapili jijini Cape Town. Lionesses walimaliza kileleni Kundi A baada ya kuipepeta Colombia 12-5, Uganda 10-5 na Ubelgiji 17-5 kabla ya kutinga fainali mzima mzima. Masimba jike hao wa Kenya wanaotiwa makali na kocha Dennis Mwanja, na ambao walishinda duru ya kwanza jijini humo mnamo Machi 2, waliwapeleka mchakamchaka wenyeji Afrika Kusini na kuwazaba mikimbio 17-0 kwenye fainali yake ya aina yake iliyopigwa Jumapili katika Uwanja wa Michezo wa Athlone.

Miguso ya Naomi Amuguni, Sharon Auma na Freshia Oduor ilitosha kuzamisha jahazi la Women Boks wa Afrika Kusini, huku msumari wa mwisho kwenye jeneza la wageni likishindiliwa na Sinaida Nyachio.
Riadha: Wakenya watamba Japan na Ufaransa
Katika riadha, nyota wa mbio za masafa, Sheila Chepkirui aliiweka Kenya kwenye ramani ya dunia baada ya kubeba taji la mbio za wanawake pekee za Nagoya Marathon nchini Japan, Jumapili. Chepkirui, 34, ambaye alishinda New York Marathon nchini Amerika mwaka jana, aliwatoka wapinzani wake wa karibu Sayaka Sato (Japan) na Eunice Chumba (Bahrain) mzawa za Kenya, zikisalia kilomita sita na kukata utepe wa mbio hizo za kilomita 42 kwa saa 2:20:40.

Chepkirui amezoa kitita cha Dola za Amerika 250,000 za Marekani sawa na Shilingi milioni 32 za Kenya kwa ushindi huo. Nchini Ureno, Wakenya Ruth Chepngetich na Shadrack Kipkemei waliridhika na nafasi ya pili na tatu kwa usanjari huo katika mbio za Lisbon Half Marathon. Mhabeshi Tsigie Gebreselama aliibuka malkia kwa kukamilisha 21km kwa saa 1:04:21 akifuatiwa na Chepngetich (1:06:20) na Mswidi Abeba Aregawi (1:06:36). Na huku nchini Ufaransa, Kennedy Kimutai (1:00:16), Timothy Kosgei (1:00:22) na Timothy Kibet (1:00:44) walifagia nafasi tatu za kwanza za wanaume za Paris Half Marathon nao Jackline Cherono (1:07:16) na Christine Kioko (1:09:55) wakawa nambari moja na tatu kwa upande wa kinadada.
Debi la Kariakoo lapigwa STOP!
Kamati ya Usimamizi na Uendesha ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza rasmi kuakhirisha mchezo wa Ligi Kuu namba 184 kati ya Yanga SC dhidi ya Simba SC uliyopangwa kuchezwa Jumaosi jioni. Bodi imefanya maamuzi hayo baada ya kupokea taarifa ya awali ya Ofisa Usalama wa Mchezo ambayo imeanisha matukio kadhaa yaliyopekea Simba SC kushtaki kwa TFF na Bodi ya Ligi kutokana na kushindwa kufanya mazoezi. Bodi ya Ligi imesema mchezo huo utapangiwa tarehe nyingine baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa kina kuhusiana na sababu zilizosababisha mchezo huo kutochezwa. Awali, licha ya klabu ya Simba kutoa tamko la kususia kuleta timu uwanjani kwenye mchezo huo wa derby ya Kariakoo uliopangwa kuchezwa Jumamosi ya Machi 8, kufuatia kikosi chake kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilitoa tamko kwamba mechi hiyo ipo palepale kama ilivyopangwa. Suitofahamu hii imewaacha hoi mashabiki wengi wa watani hao wa jadi ambao walikuwa wanaisubiri mechi hiyo kwa hamu na shauku kubwa.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Yanga SC, Arafat Haji, ameweka wazi kuwa mechi ya watani wa jadi kati ya Yanga SC na Simba SC, iliyokuñwa imepangwa kufanyika Machi 8, 2025, haitapangiwa tarehe nyingine baada ya kuahirishwa. Kupitia ujumbe wake kwenye Instagram, Arafat amewapongeza mashabiki wa Yanga kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani kutoka maeneo mbalimbali nchini, akitambua juhudi zao za kusafiri kwa njia tofauti ili kushuhudia mchezo huo.
Mbinyo dhidi ya wachezaji Waislamu Ufaransa
Wachezaji wa soka Waislamu nchini Ufaransa wamepigwa marufuku kufunga wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani wanapokuwa wakifanya mazoezi na timu ya taifa. Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) limeanzisha marufuku hiyo, hali iliyozua shutuma za ubaguzi na kuleta mgawanyiko ndani ya timu. Taarifa zinasema shirikisho hilo limewaambia wachezaji wanaofunga suamu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa hawawezi kufunga wakiwa katika kambi ya mazoezi ya Clairefontaine. Badala yake, wanaweza kufidia siku zao za kufunga baada ya kumalizika mechi za kimataifa. "Marufuku ya hijabu kwa wanawake, na sasa marufuku ya kufunga kwa wachezaji wanaofunga Ramadhani. Ufaransa inaendelea kuwa bingwa wa sera za chuki dhidi ya Waislamu," alisema mwandishi wa habari za michezo wa Kanada, Shireen Ahmed, kupitia mtandao wa X (Twitter). Wachezaji wengi wa Les Bleus ni wenye asili ya ya Afrika, wakiwemo Ousmane Dembélé, N’Golo Kanté, Elias Guendouzi, Ibrahima Konaté na Ferland Mendy. Mwaka jana, kiungo chipukizi Mahamadou Diawara alijiondoa katika kikosi cha wachezaji wa chini ya miaka 19 kwa kupinga marufuku hiyo, kulingana na taarifa ya ESPN. Hii si mara ya kwanza kwa FFF kuzua utata. Mwaka jana, marefa waliamriwa wasisimamishe mechi wakati wa magharibi ili wachezaji wanaofunga waweze kufuturu. Hii ilitofautiana na ligi kama Premier League ya Uingereza na Bundesliga ya Ujerumani, ambazo ziliwaruhusu wachezaji kufuturu. Mbali na marufuku ya kufunga, FFF pia inazuia wachezaji wa kike kuvaa hijabu, hata baada ya FIFA kuondoa marufuku yake yenyewe.
Kriketi: India yaikate ngebe New Zealand
New Zealand ilishindwa kufurukuta mbele ya India kwenye fainali ya Champions Trophy 2025 ya Baraza la Kimataifa la Kriketi ICC huko Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu. India iliibuka kidedea kwenye mashindano hayo ya kimataifa ya kriketi kwa wiketi nne dhidi ya New Zealand katika fainali ya Kombe la Mabingwa huko Dubai. Rohit Sharma aliongoza msururu huo akiwa na 76 kati ya mipira 83 na KL Rahul ambaye hajapoteza mikondo 34 aliisaidia India kuvuka mstari wa mwisho kwa mikimbio 254-6 na kushinda Kombe la Mabingwa Jumapili kwa mara ya tatu sasa. Ushindi huo ulikuwa wa 23 kwa India katika michezo 24 katika mashindano matatu ya mwisho ya ICC kwa upande wa wanaume kuanzia 2023 – ambapo imepoteza pekee dhidi ya Australia katika fainali ya Kombe la Dunia la Kriketi la 2023.

New Zealand ilikosa huduma za mchezaji wake mashuhuri, Matt Henry ambaye alikosa mechi hiyo kutokana na jeraha. Dubai ndio walikuwa wenyeji wa fainali hiyo baada ya India kukataa kusafiri kwenda kwa taifa mwenyeji, Pakistan. India haijashindwa katika mchuano huo na ndio timu pekee iliyoishinda New Zealand katika mchujo wao wa hatua ya makundi. Timu zote mbili zimeshinda mashindano hayo hapo awali, India mwaka 2002 na 2013 na New Zealand mnamo 2000.
EPL; Arsenal na Man U nguvu sawa
Na katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, watani wa jadi klabu za Arsenal na Manchester United walitoshana nguvu kwenye mchuano wa kukata na shoka Jumapili, ambapo Mashetani Wekundu walikuwa wanaupigia nyumbani Old Trafford. Gunners walitawala mchezo huo tokea mwanzo hadi mwisho licha Man U kutangulia kuona lango lao. Bao United lilifungwa na Bruno Farnandes kabla ya kupulizwa kipyenga cha kumaliza kipindi cha kwanza, huku Wabeba Bunduki wakiyatua risasi ya kuweka mambo sawa bin sawa kunako dakika ya 74, kupitia bao na Declan Rice. Arsenal kwa sasa wanaendelea kutulia katika nafasi ya pii jedwalini wakiwa na alama 55, pointi 15 nyuma wa mibabe Liverpool, ambao waliigaragaza Southampton mabao 3-1 ugani Anfield. Chelsea ambao waliitandika Leicester bao moja la uchungu bila jibu, wapo katika nafasi ya nne wakiwa na alama 49, wakibebwa na Nottingham Forest wenye pointi 51. Orodha ya tano bora kwa sasa inafungwa na City wenye alama 47.
.......................MWISHO.................