Ulimwengu wa Spoti, Apr 7
Hujambo mskilizaji mpenzi mwanaspoti. Ufuatao ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia.
Soka Ufukweni: Iran yapongezwa
Maafisa mbali mbali wa Iran wameendelea kuipongeza timu ya soka ya ufukweni ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kutamalaki tena fainali za Kombe la Asia la AFC kwenye mchezo huo, baada ya kutetea taji lake kwa ushindi mnono wa mabao 8-1 dhidi ya Oman katika fainali ya Thailand 2025. Kocha mkuu wa timu ya soka ya ufukweni ya Iran, Ali Naderi alisema, "Ushindi huo ni ushahidi wa bidii na kujitolea kwa wachezaji wetu, ambao wameonyesha utendakazi wa pamoja na ustadi katika muda wote wa mashindano. Tunajivunia kurudisha kombe hili la kifahari tena nchini Iran."

Ofisi ya Rais wa Iran imesema katika ujumbe wake wa tahania kuwa: Ubabe wa timu ya taifa ya Iran barani Asia unaashiria uwezo wa nchi hii katika kukuza vipaji vya hali ya juu licha ya changamoto katika nyanja za kimataifa na ndani. Lilikuwa tukio la kihistoria kwa Iran, kwani sio tu waliibuka mabingwa mfululizo kwa mara ya kwanza, lakini ushindi huo unawaweka mbele ya Japan kama mabingwa mara nne pekee. Wakati huo huo, Iran imefahamu wapinzani wake kwenye Kombe la Dunia la Soka la Ufukweni la FIFA 2025. Vijana hao wanaonolewa na Ali Naderi wamepangwa kwenye pote moja na mabingwa mara mbili wa Ureno, Mauritania na Paraguay.
AFC U17; Iran sare na Korea Kaskazini
Timu za soka za vijana za Iran na Korea Kaskazini zilitoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mechi ya Kundi D ya mashindano ya AFC kwa vijana wenye chini ya miaka 17 ya Saudi Arabia 2025 Jumamosi. Shinikizo la mapema la vijana wa Korea Kaskazini lilizawadiwa katika dakika ya nane baada ya Choe Chung Hyuk kufunga kwa kichwa akimalizia mpira wa kona wa Pak Kwang Song. Katika dakika ya 24, Iran ilipata bao la kusawazisha baada ya shuti la mbali la Mehdi Sahneh kumpita Kim Tae Guk, na kumuacha hoi kipa wa Korea, Jong Hyon Ju.

Matokeo hayo yameziacha timu zote mbili nyuma ya Tajikistan - ambayo iliifunga Oman mabao 2-1 mapema siku hiyo ya Jumamosi. Iran itamenyana na Oman katika mechi ijayo wakati ambapo Korea Kaskazini itakuwa inatoana udhia na Tajikistan, mechi zote mbili zikipigwa Jumanne.
Persepolis na Esteghlal zaomboleza
Klabu za soka za Iran za Esteghlal na Persepolis zinaomboleza kifo cha mchezaji wao wa zamani mwenye asili ya Afrika. Jacques Elong Elong, kiungo wa zamani wa timu hizo alifariki dunia katika ajali ya barabarani hivi karibuni.
Mchezaji huyo wa kati safu ya ulinzi aliyekuwa na umri wa miaka 40, alijiunga na Persepolis mwaka 2005 kabla ya kwenda Sepahan baada ya miaka mitatu. Raia huyo wa Cameroon pia alizichezea timu za Iran ya Esteghlal na vile vile Paykan. Elong Elong aliwakilisha timu ya taifa ya kandanda ya Cameroon kuanzia 2006 hadi 2010.
Serengeti yaaga AFCON U17 baada ya kulazwa na Uganda
Kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Uganda kumeifanya timu ya taifa ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 17 ya Tanzania 'Serengeti Boys' kuwa timu ya kwanza kuaga fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo (AFCON U17) zinazoendelea Morocco. Maumivu kwa Serengeti Boys hayajaishia kwa wao kutolewa tu, bali pia kupoteza rasmi fursa ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Qatar baadaye mwaka huu. Mabao ya Simon Manyama, Richard Okello na James Bogere katika kipindi cha pili, yalimaanisha kuwa Serengeti Boys haiwezi kufikisha pointi na hivyo haitoweza kutinga robo fainali.

Katika mchezo wake wa kukamilisha ratiba dhidi ya Morocco Jumapili ya Aprili 6, Serengeti Boys walibamizwa mabao 3-0. Uganda hiyo pia wikendi ilipata ngoma size yake, baada ya kuchabangwa na Zambia mabao 2-1, wakati ambapo Afrika Kusini ilikuwa ikipokea pia kichapo cha mbwa cha mabao 3-0 kutoka Burkina Faso.
Samia Cup; Dream FC kidedea
Timu ya soka ya Dream FC ya Ferry Kigamboni ya Tanzania imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Samia Cup kwa kuichapa Wahenga FC mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa Jumamosi ya Aprili 5 kwenye Uwanja wa Mji Mwema, jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Twende Pamoja na Mama Sports Promotion chini ya Mkurugenzi wa Makunduchi Villa, Mohammed Hajji maarufu Boss Mo yalianza Februari 7, 2025 yakishirikisha jumla ya timu 32 kutoka maeneo mbalimbali ya jijini humo. Akizungumzia mashindano hayo, mgeni rasmi wa mechi ya fainali, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga amewapongeza waandaaji wa michuano hiyo kwa kufanya jambo katika kusheherekea miaka minne ya utawala wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Amesema mashindano hayo yanasaidia kuibua vipaji, huku akiwaomba waandaaji hao kufanya mashindano mengine yatakayohusisha wanawake hasa netiboli.
Tanbihi; Klabu ya soka ya Simba ya Tanzania itavaana na Waarabu wa al-Masry ya Misri katika mechi ya marudiano ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Aprili 9. Wekundu wa Msimbazi wanalazika kuvuna ushindi wa angalau mabao 3-0, kwa kuzingatia kuwa walinyolewa ugenini kwa kuzabwa mabao 2-0. Timu inayofuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika inakuwa na uhakika wa kuzoa kiasi cha Dola 750,000 kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Raga: Kenya yamaliza ya pili Singapore 7s
Timu ya taifa ya raga ya Kenya ya wachezji saba kila upande, Shujaa Sevens ilishindwa kufurukura kwenye mchezo za fainali za Singapore Sevens siku ya Jumapili dhidi ya Fiji. Shujaa walitunukiwa medali ya fedha baada ya kuibuka mshindi wa pili kwenye fainali hiyo. Naam, ingekuwa tamu zaidi ikiwa Shujaa wangerudia ushujaa wao wa 2016 walipoiduwaza Fiji kwa kuilaza 30-7 na kushinda mechi yao pekee ya HSBC, Singapore Sevens.

Hata hivyo, historia haikujikariri siku ya Jumapili. Licha ya kuongoza kwa mikimbio 7-0 katika kipindi cha kwanza, Shujaa ambao walitinga fainali baada ya kuitufulia mavumbi Uhispania, walilaza damu katika kipindi cha mwisho na kushindwa kwa 21-12 baada ya kugusa majaribio matatu. Licha ya Shujaa kushindwa kwenye fainali hizo, lakioni wanarejea nyumbani kifua mbele baada ya kupoteza mechi moja pekee kwenye mashindano hayo ya dunia, mechi hiyo ya fainali.
Riadha: Wakenya na Waethiopia wawika tena
Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya kilomita 10, Agnes Jebet Ngetich aliitoa Kenya kimasomaso baada ya kuibuka wa pili kwenye mbio za mita 3000 kwa wanawake katika mashindano ya Kingston Marathon nchini Jamaica siku ya Ijumaa. Ngetich alimaliza nyuma ya Muethiopia Ejgayehu Taye, mshindi wa medali ya shaba ya dunia ya mita 3000 ya mwaka 2022, ambaye alikata utepe wa ushindi kwa kutumia dakika 8:28.42 huku nyota huyo wa Kenya akitumia 8:28.75, huku bingwa mara mbili wa Olpimiki katika mbio za mita 10,000 Tsige Gebreselama, pia kutoka Ethiopia akifunga orodha ya tatu bora. Naye mwanariadha nyota wa Kenya Lilian Kasait alifanya kweli Jumamosi katika mbio za Prague Half Marathon nchini Czech, baada ya kushinda mbio hizo za nusu-marathon kwa kutumia saa moja, dakika 05 na sekunde 27. Wanariadha wa Kenya na Ethiopia waling'ara pia katika mbio za Berlin Half Marathon na Hannover Marathon nchini Ujerumani, Milan Marathon (Italia), Madrid Half Marathon (Uhispania) na Sao Paulo Marathon (Brazil).
.......................TAMATI..................