Aug 08, 2023 07:46 UTC
  • IRGC: Iran itatoa jibu la aina yake kwa hatua yoyote ghalati ya Marekani katika eneo

Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) ameitahadharisha Marekani dhidi ya kuchukua hatua yoyote ghalati na ya uharibifu katika eneo la Asia Magharibi, ikiwemo kutwaa meli zinazopita katika maji ya eneo hili.

Brigedia Jenerali Ramezan Sharif amenukuliwa akisema hayo na Press TV na kuongeza kuwa, "Iran imefikia kilele na upeo wa nguvu na uwezo mkubwa kwa kadri kwamba inaweza kutoa jibu la aina yake kwa kitendo na hatua yoyote ghalati ya Marekani (katika eneo) kukiwemo kutwaa meli."

Kamanda huyo mwandamizi wa IRGC amebainisha kuwa: Katika makabiliano ya moja kwa moja baina ya Marekani na Iran katika miaka ya hivi karibuni, nchi za eneo zimeshuhudia udhaifu wa Marekani na nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu; na zikaelewa kuwa usalama wa Ghuba ya Uajemi unaweza tu kudhaminiwa na nchi zinazopakana (na Ghuba hiyo)."

Kauli ya Msemaji wa Jeshi la IRGC la Iran imekuja baada ya Marekani kutuma askari 3,000, ndege za kivita na manowari za kijeshi Asia Magharibi,  kwa kisingizio cha kutoa ulinzi kwa meli za kibiashara zinazopita katika maji ya Ghuba ya Uajemi, ikiwa ni hatua nyingine ya kichokozi na uingiliaji wa kijeshi katika eneo hili la kistratejia.

Vikosi vya majini vya Iran katika Ghuba ya Uajemi

Jumamosi iliyopita pia, Abolfazl Shekarchi, Msemaji wa Jeshi la Iran alisema usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Bahari Hindi hauna mfungamano wowote na Marekani.

Alisema nchi za eneo la Asia Magharibi zina uwezo wa kudhamini usalama wa maji ya kanda hii, pasi na kuhitaji msaada wa Marekani. Shekarchi aliihubutu Washington kwa kuhoji kuwa: Usalama wa Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Bahari Hindi una mfungamano gani na Marekani? Vikosi vya Marekani vinafanya nini katika eneo?"

Tags