Oct 10, 2023 07:04 UTC
  • Iran na Sudan kufungua tena balozi zao baada ya kukamilisha mchakato wa kuhuisha uhusiano

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, karibuni hivi Iran na Sudan zitafungua tena balozi zao baada ya nchi hizo mbili kukamilisha mchakato wa kurejesha uhusiano wa kidipolmasia.

Kwa mujibu wa Hussein Amir-Abdollahian, Iran na Sudan zilikubaliana jana Jumatatu kurejesha uhusiano wa kidiplomasia. Taarifa ya pamoja ya Khartoum na Tehran imesema, pande mbili zimefikia makubaliano ya kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia baada ya kukatwa kwa miaka saba. Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kupita miezi mitatu tangu kulipofanyika mkutano kati ya mawaziri wa mashauri ya Kigeni wa Iran na Sudan.

Nchi hizo mbili zilitoa taarifa ya pamoja hapo jana, ambayo inasema kurejeshwa kwa uhusiano huo kunafuatia makubaliano yaliyofikiwa jana hiyo hiyo baada ya harakati za muda mrefu za maafisa kutoka pande zote mbili.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imesema, pande hizo mbili zimeafikiana kuimarisha ushirikiano katika maeneo tofauti ambayo yanaweza kukidhi maslahi ya mataifa yote mawili na kuhakikisha usalama na utulivu katika eneo.

Bendera za Iran na Sudan

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ilieleza pia kwamba, pande mbili zimekubaliana kuhuisha tena uhusiano wa kirafiki baina yao kwa msingi wa kiila mmoja kuheshimu mamlaka ya kujitawala mwenzake, usawa, maslahi ya pamoja na kuishi kwa amani na usalama.

Iran na Sudan zimekubaliano pia kuchukua hatua zinazohitajika kwa ajili ya kufungua balozi zao mjini Tehran na Khartouum katika siku za usoni.

Tags