Oct 17, 2023 12:01 UTC
  • Kiongozi Mkuu wa Iran: Jinai za Gaza zisiposimamishwa, hakuna atakayeweza kuwazuia Waislamu na Wanamuqawama

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: wananchi wa mataifa ya Kiislamu na hata watu wasio Waislamu duniani wamekasirishwa sana na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala unaoikalia Quds kwa mabavu, na iwapo unyama na ushenzi huo utaendelea Waislamu duniani na vikosi vya Muqawama wataishiwa na subira na hakuna atakayeweza kuwazuia.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo alikuwa na mkutano na wenye vipawa na wasomi wenye vipaji vya juu vya Sayansi nchini, ambapo aliashiria jinai za utawala wa Kizayuni za mauaji ya kimbari unayofanya dhidi ya wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na akasisitizia ulazima wa kusitishwa mashambulio ya utawala huo ghasibu.
Ayatullah Khamenei amesema, yanayojiri hivi sasa Palestina ni jinai za dhahiri shahiri za utawala wa Kizayuni na mauaji ya wazi ya kimbari unayofanya mbele ya macho ya walimwengu wote; na akaashiria nafasi ya Marekani katika upangaji sera za hatua zinazochukuliwa na Wazayuni na akasema: "malalamiko waliyotoa maafisa wa baadhi ya nchi katika mazungumzo na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kwamba kwa nini Wapalestina wameua raia? Kauli hii haina ukweli kwa sababu wakazi wa vitongoji sio raia na wana silaha, lakini hata kama tutachukulia kuwa ni raia, ni wangapi kati yao waliuawa na ni raia wangapi wa Palestina wameuawa shahidi katika siku hizi"?
Ayatullah Khamenei akihutubia hadhara ya wenye vipawa na wasomi wenye vipaji vya juu vya Sayansi nchini

Ayatullah Khamenei ameongezea kwa kusema: utawala ghasibu wa Israel umeua mara mia zaidi ya idadi hiyo, yaani katika siku hizi chache, maelfu kadhaa ya wanawake, watoto, wazee na vijana raia wa kawaida wameuliwa shahidi; na unaendelea kutenda jinai mbele ya walimwengu kwa kushambulia kwa mabomu vituo na majengo ambayo unajua kwamba ni makazi ya raia.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, ni lazima utawala ghasibu wa Kizayuni ufunguliwe mashitaka kutokana na jinai kadha wa kadha unazofanya dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina; na serikali ya Marekani ndiyo inayobeba dhima ya sera zinazotekelezwa na utawala huo ghasibu na akaongeza kuwa: "kwa mujibu wa taarifa kadhaa, Wamarekani ndio wapangaji na waratibu wa sera zinazotekelezwa siku hizi na utawala ghasibu (Kizayuni) na kwa hivyo Marekani inabeba jukumu katika kadhia hii na inapaswa iitambue dhima yake".
Taswira ya jinai na unyama unaofanywa na Wazayuni Gaza kwa uungaji mkono wa Marekani na Ulaya

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa mashambulio dhidi ya Ukanda wa Gaza lazima yakomeshwe mara moja; na akaielezea mikusanyiko ya wananchi wa mataifa ya Waislamu katika nchi za Kiislamu na hata zisizo za Waislamu huko Marekani na Ulaya kuwa ni ishara ya kughadhabishwa mno mataifa hayo na jinai za utawala wa Kizayuni; na akaeleza bayana kwamba: "ikiwa jinai hizi zitaendelea, Waislamu na vikosi vya Muqawama wataishiwa na subira na hakuna atakayeweza kuwazuia".

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: bila shaka hata utawala wa Kizayuni ufanye nini, hauwezi kufidia kipigo na kushindwa kulikoufedhehesha katika operesheni ya "Kimbunga cha  Al-Aqsa.../

 

Tags