Katika mkesha wa kufanyika safari ya pili ya Rais Raisi nchini Russia
(last modified Wed, 06 Dec 2023 11:44:13 GMT )
Dec 06, 2023 11:44 UTC
  • Katika mkesha wa kufanyika safari ya pili ya Rais Raisi nchini Russia

Kesho Alhamisi, Rais Raisi Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku akiwa anaongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi, ataondoka nchini kuelekea Moscow kwa mwaliko rasmi wa Rais Vladimir Putin wa Russia.

Mashauriano kuhusu masuala ya pande mbili yakiwemo maingiliano ya kiuchumi na pia mazungumzo kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa hususan kadhia ya Palestina na matukio ya Gaza yatakuwa ajenda kuu ya mazungumzo ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika safari hiyo ya siku moja.

Hii ni safari ya pili kufanywa na Rais Raisi nchini Russia tangu tangu alipoingia madarakani. Katika safari yake aliyofanya mjini Moscow tarehe  22 Disember 2021 Rais Raisi aliashiria katika mazungumzo yake na Rais Vladimir Putin nafasi yenye ushawishi mkubwa ya nchi  mbili katika eneo na upeo wa kimataifa. Alisema misimamo inayofanana ya nchi mbili kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa ni msingi mzuri wa kuimarishwa ushirikiano wa pamoja na kuongeza kuwa uhusiano wa Iran na Russia uko kwenye njia ya uhusiano wa kistratijia. Hivi sasa, safari ya pili ya Raisi nchini Russia inafanyika huku Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, akikutana hapo siku ya Jumanne pembezoni mwa kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi jirani za Bahari ya Caspian mjini Moscow na Sergei Lavrov, Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Russia, ambapo pande mbili zilitia saini makubaliano ya kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja vya nchi za Magharibi.

Rais Vladimir Putin wa Russia

Nchi zote mbili za Iran na Russia ziko chini ya vikwazo vya nchi za Magharibi, hasa Marekani, suala ambalo limeongeza azma ya Tehran na Moscow ya kuendeleza ushirikiano mpana na wa muda mrefu, ikiwa ni pamoja na uhusiano wa kibiashara na kiuchumi, hasa katika kukamilisha mradi wa korido ya Kaskazini-Kusini na kukamilisha miundombinu.

Kuhusiana na hilo, Sergei Lavrov amesisitiza umuhimu wa korido hiyo na kusema Russia inataka kuongeza uwezo wa ukanda huo na pia kupanua maingiliano na Iran katika uga wa nishati. Kuanzia mwaka 2020 hadi 2022, mabadilishano ya kibiashara kati ya Iran na Russia yameongezeka zaidi ya mara mbili na kufikia dola bilioni 4.6 mwaka 2022, kutoka dola bilioni 2.22 mwaka 2020. Katika miezi 9 ya kwanza ya 2023, mabadilishano ya kibiashara kati ya Russia na Iran yameongezeka kwa asilimia 30 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita, wakati kwa mujibu wa Kazem Jalali, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Moscow, kwa sasa asilimia 60 ya biashara kati ya nchi hizi mbili inafanyika kwa kutumia sarafu za kitaifa za ruble na riali.

Kwa hakika misimamo ya pamoja ya Iran na Russia kuhusu matukio mengi ya kieneo na kimataifa, ukiwemo upinzani dhidi ya siasa za mabavu na za upande mmoja za Marekani, masuala ya Asia ya Kati, Caucasus, Afghanistan, Yemen, Iraq na Syria na kupambana na ugaidi, yanaonyesha kuwa Iran na Russia zina maslahi ya pamoja ya kistratijia katika mahusiano yao ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama.

Matukio ya Palestina na vita vya Gaza ni miongoni mwa mambo mengine ambayo viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Shirikisho la Russia wanaendelea kuyazingatia kwa karibu licha ya kuwepo hitilafu za mitazamo kuhusiana na utawala wa Kizayuni. Katika wiki za hivi karibuni, kufuatia mashambulizi ya kikatili ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, marais hao pamoja na mawaziri wao wa mambo ya nje wamefanya mashauriano kwa njia ya simu na kusisitiza ulazima wa kusitishwa jinai za Wazayuni na kutolewa misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina wanaoishi Gaza.

Jinai za Wazayuni Gaza

 

Kwa kuzingatia hayo, suala la matukio ya Gaza ni miongoni mwa masuala ambayo yamo katika ajenda ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika safari yake nchini Russia ambapo atakutana na kufanya mazungumzo na Rais Vladimir wa nchi hiyo.

Katika mazungumzo ya simu na Rais wa Russia tarehe 16 Oktoba, Rais Raisi alitathmini vizuri misimamo ya nchi hiyo katika kulaani jinai za kivita za utawala wa Kizayuni huko Gaza na kusema: “Kulingana na kinachoendelea Gaza, kuna uwezekano wa kupanuka wigo wa vita na mizozo katika nyanja nyingine, na hili likitokea, itakuwa vigumu kudhibiti hali hiyo. Hivyo tunatarajia kuwa nchi zote na mashirika ya kimataifa yatatekeleza majukumu yao, na Russia ikiwa miongoni mwa nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, itakuchukua hatua muhimu zaidi katika kukomesha jinai za kivita za utawala wa Kizayuni."