WHO yaonya kuhusu vifo vya wagonjwa huko Gaza
-
WHO: Wapalestina 900 wameaga dunia Gaza kutokana na kuchelewa kupata huduma za matibabu
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, kushindwa kupata vibali vya kuondoka mara moja kwa wagonjwa kutoka Gaza kumesababisha vifo vya wagonjwa 900 hadi sasa.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa wagonjwa wasiopungua 16,500 katika Ukanda wa Gaza wanasubiri kupelekwa nje kwa ajili ya matibabu na kusisitiza kuwa suhula zake za tiba ziko tayari mpakani lakini haziwezi kuingia katika eneo hilo kufuatia Israel kufunga vivuko hivyo.
Shirika hilo limeonya kuwa kucheleweshwa wagonjwa kuondoka Gaza kwa ajili ya kwenda kupata matibabu nje ni sawa na hukumu ya kifo.
Tedros Adhanom Ghebreyesus Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani ametoa tangazo hilo na kutoa wito wa kufunguliwa mara moja vivuko vyote na kuruhusu watu kuingia na kutoka nje ya nchi bila vizingiti kwa madhumuni ya matibabu na kibinadamu.
Kufunga vivuko na kuzuia wagonjwa kuondoka Gaza kumesababisha kuporomoka hali ya afya na kuzorotesha zaidi hali ya wagonjwa.
Wakati huo huo, hospitali za Gaza zinafanya kazi chini ya nusu ya uwezo wao kutokana na uhaba wa dawa, mafuta na vifaa vya kimsingi.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Umoja wa Maataifa umetangaza mara kwa mara kuwa, ukwamishaji wa Israel unaendelea kuzuia usmabazaji wa misaada ya kibinadamu kuelekea Ukanda wa Gaza yapata mwezi mmoja sasa tangu Telv Aviv na harakati ya muqawama ya Palestina Hamas zitekeleze makubaliano ya kusitisha mapigano.