Iran yatuma vikosi na zana za kijeshi katika mpaka wa kaskazini
(last modified Mon, 18 Dec 2023 11:11:14 GMT )
Dec 18, 2023 11:11 UTC
  • Iran yatuma vikosi na zana za kijeshi katika mpaka wa kaskazini

Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Iran ametangaza habari ya kutumwa wanajeshi na zana za kivita katika mpaka wa kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kiislamu ili kupiga jeki operesheni za kukabiliana na makundi ya kigaidi yalioazimia kuvuruga usalama wa taifa hili.

Brigedia Jenerali Kioumars Heidari amesema hayo leo Jumatatu na kuongeza kuwa, lengo la kutumwa vikosi zaidi katika maeneo hayo ya mpakani ni kuzuia kujipenyeza nchini magaidi kutoka nchi jirani.

Amesema kikosi hicho kinachojumuisha wanajeshi waendao kwa miguu, kwa kutumia zana mbali mbali kama makombora na ndege zisizo na rubani (droni) kimejiandaa barabara kutoa jibu kwa vitisho vya aina yoyote dhidi ya Iran.

Kamanda Heidari ameeleza bayana kuwa,  vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hii vitaendelea kulilinda taifa hili kutokana na vitisho vya kutoka nje ya mipaka yake.

Wakati huo huo,  Naibu Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Iran amesema vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hii vipo macho na vimejiandaa kukabiliana na tishio lolote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Brigedia Jenerali Kioumars Heidari

Brigedia Jenerali Mahdi Hadian amebainisha kuwa, utayarifu wa hali ya juu wa vikosi vya nchi hii umepelekea maadui kukata tamaa na kutokuwa na mawazo yoyote ya kulishambulia kijeshi taifa hili.

Haya yanajiri siku chache baada ya viongozi na maafisa mbalimbali wa Iran sambamba na kulaani shambulio la kigaidi lililosababisha mauaji ya maafisa 12 wa polisi wa Jamhuri ya Kiislamu huko Rask, kusini mashariki mwa Iran kusema kuwa, shambulio hilo la kikatili litalipiziwa kisasi haraka sana. 

Mwishoni mwa mwaka uliopita, Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kilituma wanajeshi zaidi katika mipaka ya magharibi na kaskazini magharibi mwa Iran ili kukabiliana na makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga, yaliyoko katika eneo la Kurdistan ya Iraq.

Tags