Raisi: Iran inaunga mkono kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel ICJ
Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono uamuzi wa 'busara' na wa 'kihistoria' wa Afrika Kusini wa kuwasilisha kesi dhidi ya utawala haramu wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kuhusu jinai za mauaji ya kimbari zinazotekelezwa na utawala huo dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Rais Ebrahim Raisi alisema hayo jana Jumapili katika mkutano wake na Balozi mpya wa Afrika Kusini hapa mjini Tehran, Francis Molloy wakati mwanadiplomasia huyo akimkabidhi Rais wa Iran vyeti vyake vya utambulisho.
Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa: Hatua ya Afrika Kusini ya kulalamikia jinai za utawala wa Kizayuni (wa Israel) ni ya kihistoria, ya kudumu na ya kupongezwa, na Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono uamuzi huu wa busara.
Kadhalika Rais wa Iran ameashiria uhusiano mzuri na uliokita mizizi baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Afrika Kusini na kusisitiza kuwa, hakuna kikwazo chochote cha kuzuia kuimarishwa zaidi uhusiano huo wa pande mbili.
Afrika Kusini ilifungua kesi dhidi ya Israel mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka uliomalizika, baada ya takriban miezi mitatu ya vita vya maangamizi ya umati vya Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza.
Katika nyaraka za kesi, Afrika Kusini imesema hatua za Israel ni "mauaji ya kimbari kwa sababu zina nia ya kuleta uharibifu wa sehemu kubwa ya kundi la taifa, rangi na kaumu ya Palestina."
ICJ imeshaanza kusikiliza kesi hiyo dhidi ya jinai za kivita za Wazayuni Gaza, na mbali na Iran, nchi zingine kadhaa zimetangaza kuunga mkono hatua hiyo ya Afrika Kusini.
Halikadhalika, Rais wa Iran jana Jumapili alipokea vyeti vya mabalozi wapya wa Burkina Faso, Ubelgiji, Bosnia Herzegovina, Nicaragua, na Japan hapa Tehran, ambapo katika mazungumzo na wanadiplomasia hao alisisitizia haja ya kukomeshwa jinai za utawala katili wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.