Raisi: Msingi wa uhusiano wa Iran na Afrika ni maslahi ya pamoja
(last modified Thu, 25 Jan 2024 11:13:56 GMT )
Jan 25, 2024 11:13 UTC
  • Raisi: Msingi wa uhusiano wa Iran na Afrika ni maslahi ya pamoja

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uhusiano wa Iran na Mali pamoja na nchi nyingine za Afrika si wa kisiasa na kidiplomasia tu, bali umejengeka katika msingi wa maslahi ya pande mbili na pande kadhaa.

Sayyid Ebrahim Raisi amesema hayo leo Alkhamisi hapa mjini Tehran katika mkutano wake na Waziri Mkuu wa Niger, Ali Lamine Zeine na kuongeza kuwa, Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zina historia nyeusi ya kupora utajiri na rasilimali za mataifa mengine kwa kisingizio cha kulinda haki za binadamu na kuimarisha usalama.

Rais Raisi amesema sera kuu ya serikali ya Iran ni kuimarisha uhusiano na ushirikiano na nchi za Kiafrika katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

Aidha Rais wa Iran ameashiria uhusiano mzuri na uliokita mizizi baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Niger na kusisitiza kuwa, hakuna kikwazo chochote cha kuzuia kuimarishwa zaidi uhusiano huo wa pande mbili.

Sayyid Raisi amegusia hatua zilizopigwa na Niger katika njia ya uhuru na kujikomboa na kusema, "Taifa la Kiislamu la Niger lina mustakabali wenye kung'ara kwa kuwa na azma thabiti na kutegemea uwezo wake na mali asili zake."

Amesema Iran na Niger zina historia ya jadi, na mataifa haya mawili yana uwezo wa kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyuga tofauti kama vile siasa, uchumi,  nishati, viwanda na madini.

Kwa upande wake, Ali Lamine Zeine, Waziri Mkuu wa Niger amesema nchi yake ina hamu ya kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga za kilimo, nishati, viwanda na madini.

Mohammed Mokhber, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran (kulia) akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Niger, Tehran

Ameeleza bayana kuwa, dini ya Kiislamu, kupigania uhuru na kujitawala na mapambano dhidi ya ukoloni ni mambo yanayoyakurubisha pamoja mataifa haya mawili. "Mambo haya yanayolandana, yameifanya Niger iitazame Jamhuri ya kiislamu ya Iran kama rafiki wa kutegemewa na mshirika mkubwa duniani," ameongeza Zeine.

Kadhalika Waziri Mkuu wa Niger amepongeza uungaji mkono na himaya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Gaza na Palestina na kueleza matumaini yake kuwa, mahusiano kati ya nchi hizi mbili yapo katika mkondo wa kuimarika zaidi.