Kanani ajibu matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani dhidi ya Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kanani ametaja tuhuma za Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuwa ni jaribio lisilozaa matunda la kuficha uungaji mkono wa nchi hiyo kwa utawala wa Kizayuni na kutojali ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu huko Palestina.
Nasser Kanani ameongeza kuwa: Ni kinaya kichungu kuona baadhi ya serikali za Magharibi zenye rekodi ya kuwaunga mkono kwa pande zote wavunjaji wa haki za binadamu ambazo zilihusika moja kwa moja kuufadhili na kuupatia utawala wa Saddam silaha za kemikali wakati wa vita vya kulazimishwa dhidi ya Iran na pia hivi sasa zinaunga mkono wazi wazi mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza zikitoa madai ya kutetea haki za binadamu.
Kanani ameendelea kubainisha kuwa: Viongozi wa Ujerumani wanaingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kwa kisingizio cha kulinda haki za binadamu na bila shaka kwa kulifanya suala hilo kuwa la kisiasa; huku wakikuza uchumi wa nchi yao kwa kuzidisha shughuli za viwanda vya uundaji silaha.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Hali mbaya ya Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na hali ya kutisha ya wakaazi na wakimbizi wa Kipalestina katika eneo la Rafah ni ngoma ya kashfa na uthibitisho wa wazi wa kushindwa kwa wale wote wanaodai kutetea haki za binadamu.