Wairani washukuriwa kwa kushiriki maadhimisho ya Mapinduzi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i1093-wairani_washukuriwa_kwa_kushiriki_maadhimisho_ya_mapinduzi
Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amewashukuru wananchi wa Iran kwa kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya 22 Bahman (11 Februari) kwa mnasaba wa kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2016 11:48 UTC
  • Wairani washukuriwa kwa kushiriki maadhimisho ya Mapinduzi

Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amewashukuru wananchi wa Iran kwa kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya 22 Bahman (11 Februari) kwa mnasaba wa kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Siddiqui amesema katika hotuba za Sala ya Ijumaa kuwa: "Maandamano ya tarehe 22 Bahman mwaka huu kwa mara nyingine tena yameiletea Iran fakhari kwani walimwengu wameshuhudia tena furaha na msisimko wa Wairani kwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Ameongeza kuwa: "Wananchi wa Iran wamethibitisha kuwa wangali wana azma ya kutetea na kulinda Mapinduzi ya Kiislamu na kukabiliana na madola ya kibeberu na kwamba kamwe hawatajitenga na malengo matukufu ya Imam Khomeini MA na miongozi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Imamu wa muda wa Sala ya Ijumaa Tehran pia ameashiria uchaguzi ujao wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, na Baraza la Wanazuoni Wataalamu na kusema: "Wale ambao wanatoa ahadi zisizoweza kutekelezeka katika uchaguzi ili wapate kushinda wafahamu kuwa wananchi hawawezi kuhadaika."

Hujjatul Islam wal Muslimin Siddiqui amewanasihi wanaogombea katika uchaguzi wa Februari 26 kujiepusha na kuwachafulia jina wagombea wengine. Aidha ametoa wito kwa wananchi wa Iran kuwachagua wagombea bora na wanaofaa zaidi kwa lengo la kulinda malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu na ya Imam Khomeini MA.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa pia amebainisha wasiwasi wake kuhusu ghasia na mapigano katika nchi za eneo hasa Yemen, Syria, Iraq na Bahrain na kutoa wito wa kufanyika jitihada za kumaliza vita katika nchi hizo sambamba na kuangamizwa makundi ya kitakfiri na kigaidi ili usalama na utulivu urejee.