Mar 27, 2024 07:41 UTC
  • Iran yazitaka IPU, NAM kufanya juhudi za kusitisha vita Gaza

Iran imetoa mwito kwa Jumuiya ya Kimataifa ya Mabunge (IPU) na Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) kuchukua hatua za maana na za kivitendo kusitisha mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Mwakilishi wa Iran, Mojtaba Razakhah Yousefi ametoa mwito huo katika mahojiano na shirika la habari la Iran Press pambizoni mwa mkutano wa 148 wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mabunge (IPU) mjini Geneva, Uswisi na kueleza kuwa, uwezo wa kiutendaji wa taasisi hizo mbili za kimataifa unaweza kutumika kusitisha vita Gaza.

Amesema Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu duniani  yamepoteza maana na itibari kwa kushindwa kusimamisha mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya miezi sita sasa.

Mbunge huyo wa Iran ameuambia mkutano wa 148 wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mabunge (IPU) mjini Geneva kuwa, Iran inafuatilia kwa makini matukio ya Gaza, na inaendelea kupinga umwagaji damu katika eneo hilo lililozingirwa. 

Amesema kuendelea mashambulizi ya kikatili ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Palestina hususan katika Ukanda wa Gaza, kunapaswa kulaaniwa.

Mauaji ya kimbari Gaza

Kadhalika mwakilishi huyo wa Iran katika mkutano wa IPU ameitaka jamii ya kimataifa izuie mauaji hayo na kuchukua hatua zote muhimu za kukomesha ukatili huo.

Mojtaba Razakhah Yousefi ameashiria mauaji ya wanasayansi wa Kiirani yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni na vikwazo vya kikatili dhidi ya taifa hili na kueleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imelipa gharama kubwa kwa sera zake za kupinga mauaji ya kimbari.

Tags