Apr 15, 2024 12:02 UTC
  • Onyo la Iran kwa Marekani na Magharibi kuhusu madhara yatakayozipata zikiiunga mkono Israel

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeionya na kuitahadharisha Marekani na nchi za Magharibi juu ya kuuunga mkono kijeshi utawala wa Kizayuni na kufanya chokochoko dhidi ya Iran na kutangaza kwamba, iwapo nchi hizo zitaingilia kati katika kuuunga mkono utawala wa Kizayuni, vituo vyao vyote na maeneo yote ya maslahi yao yatashambuliwa na vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu.

Usiku wa kuamkia Jumapili ya tarehe 14 Aprili, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilijibu mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya ubalozi wake mdogo wa mjini Damascus, Syria, na kwa mara ya kwanza ikavishambulia moja kwa moja vituo vya kijeshi vya Israel kwa kutumia mamia ya makombora na ndege zisizo na rubani. Mashambulio hayo yalifanywa baada ya jamii ya kimataifa kutoonyesha msimamo wa wazi kuhusiana na shambulio hilo la kigaidi lililofanywa na utawala wa Kizayuni kinyume na sheria dhidi ya ubalozi huo mdogo wa Iran.
Mashambulio makubwa ya makombora na droni za Iran dhidi ya Israel

Mnamo tarehe Mosi Aprili, utawala wa Kizayuni ulifanya kitendo cha jinai cha kushambulia sehemu ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, kitendo cha jinai ambacho kinakinzana na Mkataba wa Vienna wa mwaka 1968, ambao unasisitiza kuhusu kinga viliyonayo vituo vya kidiplomasia. Shambulio hilo la kigaidi lilipelekea kuuawa shahidi washauri saba wa kijeshi wa Iran.

Wiki iliyopita, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran, alitamka bayana katika hotuba za Sala ya Idul-Fitri kwamba, kitendo ilichofanya Tel Aviv ni sawa na kuishambulia ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni "utaadhibiwa tu" kwa kufanya jinai hiyo.

Shambulio la Israel katika ubalozi mdogo wa Iran

Meja Jenerali Seyyed Abdul Rahim Mousavi, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia operesheni ya makombora na ndege zisizo na rubani iliyofanywa na Iran kujibu hujuma ya hivi karibuni ya kigaidi iliyofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus na kusisitiza kwamba, ikiwa viongozi wa Marekani watataka kujiingiza au kuingilia kati kwa ajili ya kuuunga mkono utawala wa Kizayuni, vituo vyao vyote na maeneo yote ya maslahi yao, hususan vituo ambavyo vitatumiwa kuanzishia mashambulio ya kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vitaandamwa moja kwa moja na operesheni za vikosi vya ulinzi vya Iran.

Meja Jenerali Mousavi ameonya kuwa, iwapo utawala haramu wa Kizayuni na waungaji mkono wake watang'ang'ania kuendeleza vitendo vyao vya kichokozi, adhabu itakayotolewa mara hii itakuwa kali na kubwa zaidi.

Onyo la Kamanda Mkuu wa Jeshi kwa chokochoko za Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran naye pia amelizungumzia hilo kwa kusema, iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel muuaji wa watoto na waungaji mkono wake watafanya harakati yoyote ya kifidhuli, watapata jibu kali na kubwa zaidi la kijeshi. Sayyed Ebrahim Raisi amesema, Tehran haitaki kushadidisha mapigano katika eneo; na kwa sababu hiyo amezionya Israel na Marekani juu ya kuanzisha chokochoko yoyote zaidi ya kijeshi katika eneo.

Onyo la Rais Raisi juu ya chokochoko za Marekani

Katika kipindi cha siku mbili zilizopita na kufuatia kufichuliwa namna madola ya Magharibi yalivyousaidia utawala wa Kizayuni katika makabiliano baina yake na Iran, maafisa waandamizi wa kijeshi na kisiasa wa Marekani na baadhi ya waungaji mkono wengine wa Magharibi wa Israel wamesisitiza kuwa tawala zao zitaendelea kuunga mkono sera za kisiasa na kijeshi za utawala huo katika eneo.

Pamoja na hayo, na kama walivyobainisha viongozi wa kisiasa na kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu, hatua ya hivi karibuni ya kijeshi ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni imechukuliwa kwa kutumia Kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa kinachohusu "Kujihami Kihalali" kujibu shambulio la kivamizi lililofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vya kidiplomasia vya Iran mjini Damascus.

Utumiaji wa haki ya "Kujihami Kihalali" na kujibu uchokozi wowote inaofanyiwa, kunaonyesha muelekeo wa kiuwajibikaji inaofuata Iran kuhusiana na manufaa na maslahi yake ya kitaifa, na vilevile kwa amani na usalama wa kieneo na kimataifa.

Kama ilivyokwisha tangaza mara kadhaa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina nia ya kugombana na nchi yoyote ikiwemo Marekani katika eneo, lakini kama nchi hiyo itafanya operesheni yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran, raia wake au maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu, Tehran itabaki kuwa na haki ya kudumu ya kutoa jibu linalostahiki dhidi ya uchokozi huo.

Ni kama ilivyotokea wakati Marekani ilipofanya shambulio la kigaidi la kumuua shahidi Jenerali Qasem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iraq Januari 2020, ambapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bila kujali nafasi ya kisiasa na kiuchumi ya Washington katika eneo na dunia, ilichukua hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa ya kuishambulia kambi ya jeshi la Marekani ya Ain al-Assad, nchini Iraq.

Msingi huu mkuu unaonyesha kuwa, iwapo nchi yoyote, utawala au kundi lolote litashambulia popote pale yalipo maslahi, mali, shakhsia na raia wa Iran, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajibu mapigo dhidi ya shambulio hilo kutokea kwenye ardhi yake.../

Tags