Apr 20, 2024 06:43 UTC
  • Nasser Kan\'ani
    Nasser Kan\'ani

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani kura ya turufu ya Marekani dhidi ya rasimu ya azimio iliyotaka Palestina ipewe uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.

Katika upigaji kura huo, nchi 12 wanachama wa Baraza la Usalama la UN zilipiga kura za kuunga mkono rasimu ya uanachama kamili wa Palestina kkatika Umoja wa Mataifa, Uswisi na Uingereza zilipiga kura ya kutopinga au kuunga mkono upande wowote; na Marekani ilikuwa nchi pekee iliyozuia kupitishwa azimio hilo kwa kulipigia kura ya veto.

Kuidhinishwa azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kunahitaji angalau kura tisa chanya bila kupingwa au kupigiwa kura ya turufu na mmoja wa wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama, yaani Marekani, Uingereza, Russia, Ufaransa na China.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kwamba hatua hiyo ya Washington imefichua sura ya kinafiki ya siasa za nje za Marekani na kutengwa Ikulu ya White House katika jamii ya kimataifa na maoni ya umma ya walimwengu kuliko wakati mwingine wowote. 

Kan'ani ameongeza kuwa: Uungaji mkono na misaada ya upande mmoja na isiyo na kikomo ya Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika nyuga za kisiasa, kiuchumi, kijeshi, kisheria na kimataifa kwa kutumia fedha za raia wa Marekani na kwa gharama ya kutoa mhanga amani na usalama wa kieneo na kimataifa katika kipindi chote cha miongo saba iliyopita sio tu kwamba havikufuadafu lakini pia vimewafedhehesha zaidi watawala wa Marekani mbele ya maoni ya umma ya ulimwengu kuliko hapo awali na kuthibitisha kwamba Marekani inapendelea na kuegemea upande mmoja.

Tags