Apr 23, 2024 12:19 UTC
  • Hossein Amir Abdollahian
    Hossein Amir Abdollahian

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kuiwekea Iran vikwazo vilivyo kinyume cha sheria, akisema kuwa watu wa Ulaya hawapaswi kufuata ushauri wa Marekani wa kuuridhisha utawala mtendajinai wa Israel.

Hossein Amir Abdollahian ameandika kwenye akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa X kwamba Umoja wa Ulaya unaharakia kuweka vikwazo zaidi kinyume cha sheria dhidi ya Iran, kwa sababu tu Jamhuri ya Kiislamu imetumia haki yake ya kujilinda dhidi ya uchokozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Akielezea masikitiko yake juu ya uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kuiwekea Iran vikwazo vipya, Amir Abdollahian ameongeza kuwa, wakati utawala ghasibu wa Israel ukiendelea kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina kwa kufanya jinai za pamoja za kivita na mashambulizi ya makombora na kuwatesa watu kwa njaa, Umoja wa Ulaya umetosheka kutoa jibu la maneno matupu, wakati ulitakiwa kuwajibika na kuchukua hatua za kivitendo dhidi ya utawala wa Israel.

Joseph Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni za Ulaya jana Jumatatu alitangaza uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kupanua vikwazo dhidi ya miradi ya kutengeneza ndege zisizo na rubani ya Iran na kusema kuwa, mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo wamekubali kupanua zaidi vikwazo dhidi ya Iran katika uwanja wa ulinzi.

Joseph Borrell

Israel Katz, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala wa Kizayuni wa Israel amekaribisha hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya na kudai kuwa, huo ni uamuzi muhimu wa kutuma ujumbe kwa Iran kwamba hauwezi kudhoofisha utulivu wa eneo Magharib mwa Asia.

Makubaliano ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ya kuiwekea vikwazo Iran yanakuja wakati utawala wa Kizayuni ukiendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza. 

Tags