Apr 24, 2024 07:19 UTC
  • Sisitizo la Rais wa Iran kwamba Palestina ni suala kuu la Ulimwengu wa Wanadamu

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwa mara nyingine tena kuwa kadhia ya Palestina ndilo suala kuu la Ulimwengu wa Wanadamu.

Rais Raisi ameyasema hayo katika moja ya hotuba alizotoa alipokuwa kwenye ziara ya siku mbili ya kuitembelea Pakistan.
Hapo kabla ilikuwa ikisisitizwa kwamba, Palestina ni kadhia kuu ya Ulimwengu wa Kiislamu; na sababu yake ilikuwa ni jukumu kuu lililopasa kubebwa kwanza na Waislamu wote, na kisha nchi za Kiislamu, kwa mtazamo wa kidini na kiitikadi.
Japokuwa jukumu na masuulia hayo yangali yako palepale, lakini baada ya kuanza vita vya sasa vya Ghaza, Palestina imevuka mpaka wa kuwa suala la Kiislamu na la kitaifa, na kugeuka kuwa suala la Utu, kwa sababu katika vita hivyo si Wapalestina wala Ghaza, bali utu na ubinadamu ndio ulioandamwa na kuhujumiwa, jambo linalowafanya wanadamu wote wawe na jukumu na masuulia ya kukabiliana na jinai na uhalifu uliofanywa, bila kujali tofauti zao za kidini na kiimani.

Kwa muktadha huo, ilitarajiwa kuwa malalamiko na maandamano yanayoendelea kufanyika duniani dhidi ya hatua za kinyama za jeshi la Israel na serikali ya kifashisti ya Netanyahu yawe mengi na makubwa zaidi kuliko tunayoyashuhudia; lakini inavyoonekana, moja ya mambo yaliyochangia hali hiyo ni habari za uwongo na chambuzi za upotoshaji vilizotoa vyombo vya habari vya Magharibi na vya Kizayuni kwa maoni ya umma kimataifa kuhusiana na dhati halisi ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na kujaribu kuionyesha Israel kama muonewa na mwathirika, wakati ukweli halisi ni kuwa operesheni hiyo ilikuwa ni ya kujihami.

Kwa hakika operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ni nembo ya vuguvugu lililochemka lenyewe na la kimaumbile la wananchi wa Palestina, la kupigania haki zao za asili na heshima ya utu wao; na pia ni mjibizo ambao haukuwa na budi kuonyeshwa dhidi ya dhulma na ukatili usio na mwisho wa wavamizi na maghasibu dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina.

Haki ya Uhalali wa Kujihami ni haki ya asili liliyonayo taifa la Palestina, likiwa ni taifa ambalo limenyimwa isivyostahiki haki ya kimsingi ya kujiamulia majaaliwa yake, sambamba na kuandamwa kila mara na uchokozi na ukiukaji wa haki za binadamu, mbali na kuvunjiwa heshima ya utu wa binadamu wake.

Jinai zinazoendelea kufanywa hivi sasa ni dhulma maradufu dhidi ya taifa ambalo limenyimwa haki zake zote za kibinadamu na heshima ya utu, ilhali ibara ya kwanza ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa inasisitiza juu ya haki ya mataifa kujiamulia majaaliwa na mustakabali wao; lakini kutokana na utawala wa Kizayuni kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina kinyume cha sheria na kuwahamishia watu wake katika ardhi hizo umekiuka na kukanyaga kwa sura ya kutisha haki ya watu wa Palestina ya kujiamulia hatima yao.
Kwa msingi huo na kwa maana halisi ya neno lenyewe, Muqawama wa taifa la Palestina dhidi ya kukaliwa kwa mabavu ardhi zao na ukiukaji wa kutisha na wa mtawalia unaofanywa dhidi ya haki zao za binadamu, ni "Kujihami Kihalali na Kisheria" dhidi ya dhulma, uvamizi na ukandamizaji.
Hali inayoendelea kushuhudiwa hivi sasa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina na hasa huko Ghaza ni mfano wa wazi wa kuvuruga usalama wa kieneo na kimataifa na ni dhihirisho la wazi la jinai na mauaji ya kimbari. Kwa hivyo, kadhia ya Palestina na kukaliwa kwa mabavu kwa muda wa miaka 75 ardhi hiyo kongwe na ya kale mbali na kuwahamisha kwa mabavu wakazi wake wengi wa asili na kuwakandamiza na kuwadhalilisha wale waliosalia huko Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, si suala la baina ya Wapalestina na Israel pekee.
Kwa kweli, hivi sasa Ghaza inakabiliwa na mauaji halisi ya Holocaust. Kwa mujibu wa takwimu za karibuni zaidi za Wizara ya Afya ya Palestina huko Ghaza, idadi ya waliouawa shahidi imeshapindukia 34,151 na idadi ya waliojeruhiwa ni zaidi ya 77,084, na idadi hizo zinazidi kuongezeka. Zaidi ya 70% ya waathirika ni wanawake na watoto.

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, utawala wa Kizayuni umefanya jinai za kila aina katika Ukanda wa Ghaza, zikiwemo jinai dhidi ya binadamu, jinai za kivita, uangamizaji kizazi na mauaji ya kimbari na kikaumu. Vitendo vya kinyama vya Israel huko Palestina na Ukanda wa Ghaza vimekiuka waziwazi na kwa kiwango cha kutisha kanuni na sheria za kimataifa za kibinadamu.

Maazimio kadhaa yaliyotolewa dhidi ya Israel katika muktadha wa ukiukaji haki za binadamu yamejaa maneno kama "miito", "lawama", "kuonyesha wasiwasi" na "kusikitishwa" pamoja na kutolewa agizo la "kuhitimisha haraka" ukiukaji wa haki za binadamu.
Hati za kimataifa, hususan Mkataba wa Nne wa Geneva na Itifaki ya Pili ya Nyongeza ya Mikataba ya Geneva kuhusu watu wanaolindwa wakati wa mapigano ya silaha, zimezielezea hatua za Israel kuwa ni ukiukaji mkubwa wa haki za huduma za kibinadamu.
Kwa mujibu wa kanuni na hati hizo, ikiwemo ya Mkataba wa Haki za Mtoto, kuna aina maalumu za hatua zilizo dhidi ya ubinadamu zinazoonekana katika jinai na ukatili waliofanyiwa watoto huko Ghaza. Utawala wa Kizayuni umefanya jinai kama vile kutumia silaha zilizopigwa marufuku, kushambulia raia na mali za raia, kushambulia skuli, misikiti, hospitali, vikosi vya uokoaji n.k. ambapo yote hayo yanahesabiwa kuwa ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.

Kwa kuzingatia kuwa haki zilizokiukwa huko Ghaza ni miongoni mwa haki za msingi za binadamu, ambazo ukiukaji wake hauhalaliki kwa namna yoyote ile, kwa hiyo kuwafuatilia na kuwafungulia mashtaka waliofanya jinai na uhalifu bila kujali utaifa wao ni jambo linalowezekana.

Hadi sasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijaweza kusimamisha mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni na kutoa azimio kuhusiana na suala hilo; na mashirika ya kimataifa yanayojigamba kuwa watetezi wa amani duniani yameshindwa kusimamisha vita na mauaji katika Ukanda wa Ghaza. 
Katika hatua hii, kuna vipaumbele vinne vya msingi ambavyo kwa uchache vinaweza kutekelezwa, navyo ni "kukomesha mashambulizi mara moja, kikamilifu na kwa sura ya kudumu", "kurahisisha, kuharakisha na kuongeza utumaji wa misaada ya kibinadamu huko Ghaza na kufungua ukanda wa kibinadamu wa kusafirisha majeruhi na wagonjwa kuelekea nje ya Ghaza", "kuondoa kikamilifu mzingiro iliowekewa Ghaza" na "kupinga vikali uhamishaji watu kwa lazima".
Hili kwa hakika ndilo jambo dogo kabisa linaloweza kufanywa na mataifa na serikali duniani kote zikiwa ni sehemu ya jamii ya wanadamu.../