Apr 24, 2024 12:26 UTC
  • Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: Taifa la Iran halitasalimu amri mbele ya sera za mabavu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Taifa kubwa na lenye historia ya miaka mingi la Iran halitasalimu amri mbele ya sera za kidhalimu na za kupenda kujitanua na litafika kwenye upeo mzuri wa mustakabali kwa kugeuza vikwazo kuwa fursa.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo mbele ya hadhara ya maelfu ya wafanyakazi na kuongeza kuwa, lengo halisi la Marekani na nchi za Magharibi katika kuiwekea Iran vikwazo na mashinikizo ni kutaka kulilazimisha taifa na mfumo wa utawala wa Kiislamu hapa nchini kusalimu amri na kutii kikamiilifu matakwa yao. Amesisitiza kuwa: Taifa kubwa na lenye historia ndefu la Iran na Jamhuri ya Kiislamu hazitasalimu amri kwa uonevu na sera za kupenda kujitanua, na litapata mustakbali mzuri kwa kugeuza vikwazo kuwa fursa za maendeleo na ustawi.

Kiongozi Muadhamu alipokutana na maelfu ya wafanyakazi 

Ayatullah Khamenei ametaja kazi na mjasiriamali kuwa ni wenza wawili katika mstari wa mbele wa vita vya kiuchumi vya maadui dhidi ya taifa la Iran na kuongeza kuwa: Kadiri wenza hao wawili  katika mapambano dhidi ya Marekani wanavyofanya kazi vizuri zaidi na kutayarishiwa mazingira mazuri ya kazi, ndivyo nchi na taifa litakavyokuwa na mafanikio zaidi. 

Ameeleza nafasi muhimu ya jamii ya wafanyakazi katika kasi ya uzalishaji na uboreshaji wa hali ya uchumi wa nchi na kusema: Hali nzuri ya jamii ya wafanyakazi itaboresha pia hali ya taifa.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ni jambo lisilowezekana kuzungumzia masuala ya kiuchumi bila ya kutilia maanani vikwazo vilivyotajwa na Marekani na Ulaya kuwa havina kifani dhidi ya Iran. Amesema: "Kuhusu lengo la kuweka vikwazo dhidi ya Iran Wamagharibi wanasema uongo kwa kuzusha masuala kama vile silaha za nyuklia, haki za binadamu na madai ya kuwa Iran inaunga mkono ugaidi." 

Akieleza migongano na visingizio vya uongo vya Wamagharibi, Ayatullah Ali Khamenei ameashiria Gaza kama mfano na kusema: Kwa maoni yao, watu wanaoshambuliwa kwa mabomu wa Gaza ni magaidi, lakini serikali habithi, bandia na katili ya Kizayuni iliyowaua kwa umati karibu watu 40,000 wakiwemo watoto elfu kadhaa ndani ya miezi sita, sio gaidi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena lengo kuu la la vikwazo vya Wamarekani dhidi ya Iran, ambalo ni kulilazimisha taifa la Iran kusalimu amri na kutii kikamilifuu matakwa ya Wamagharibi katika nyanja za kisiasa na kiuchumi na kusema: Marekanii inataka kudhibiti utajiri, heshima na sera za Iran, kama inavyofanya katika baadhi ya nchi, lakini utawala wa Kiislamu, ghera ya Kiislamu na taifa kubwa na lenye hisroria ya muda mrefu la Iran kamwe halitasalimu amri mbele ya dhulma yao.